Kimataifa

Rishi Sunak akubali kushindwa uchaguzini, Keir Starmer achukua hatamu Uingereza

Na MASHIRIKA July 5th, 2024 2 min read

LONDON, Uingereza

KEIR Starmer atakuwa Waziri Mkuu mpya wa Uingereza huku chama chake la Labour kikitarajiwa kushinda viti vingi katika uchaguzi wa ubunge.

Hii ni baada ya chama hicho kukishinda chama tawala cha Conservative, chake Waziri Mkuu wa sasa Rishi Sunak, ambacho kimedumu mamlakani kwa miaka 14.

Huku baadhi ya matokeo yangali kutangazwa baada ya upigaji kura uliofanyika Alhamisi, chama cha Labour tayari kimeshinda zaidi ya viti 326 katika bunge hilo lenye jumla ya viti 650.

Wakati huo huo, matokeo ya kura ya maoni ya wakati wa uchaguzi yanaonyesha kuwa chama hicho kitatwaa karibu viti 410.

Kufikia Alhamisi chama cha Conservative, chake Sunak, kilikuwa kimeshinda viti 70 pekee ni ilibashiriwa kuwa kingeandikisha matokeo mabaya zaidi katika historia yake ndefu.

Kwa kuwa Wabunge nchini Uingereza ndio huchagua Waziri Mkuu, ni wazi kuwa Starmer, ambaye ni kiongozi wa chama cha Labour ndiye atatunukiwa wadhifa huo.

Wadadisi wanasema wapiga kura waliadhibu chama cha Conservative kutokana na kupanda kwa gharama ya maisha, kudorora kwa huduma za umma na msururu wa sakata.

“Usiku huu, watu hapa na kote nchini wameongea na wako tayari kwa mabadiliko, ya kukomesha siasa za ushindani na kurejesha siasa zinazochukuliwa kama huduma za umma,” Starmer akasema baada ya kushinda kiti chake cha London.

“Mabadiliko yanaanza hapa….. Mmepiga kura. Sasa ni zamu yetu kuwafanyia kazi.”

Waziri mkuu Sunak alikubali kushindwa na kuahidi kumpigia simu Starmer kumpongeza kwa ushindi wake.

“Leo mamlaka yatapokezwa kwa njia ya amani na yenye utaratibu, yenye nia njema kutoka pande zote,” alisema baada ya kuhifadhi kiti chake.

“Kuna mengi ya kujifunza na kutafakari na ninawajibika kwa ushinde wa wawaniaji wengi wa chama cha Conservative….. Naomba msamaha,” akaongeza.

Licha ya kupata ushindi mkubwa, kura za maoni zimeonyesha kuna msisimko finyu kwa Starmer au chama chake.

Aidha, anaingia mamlakani wakati ambapo Uingereza ikabiliwa na msururu wa changamoto kubwa.

Viwango vya ushuru vinatarajiwa kuwa juu zaidi nchini tangu muda mfupi baada ya Vita vya Pili vya Dunia huku mzigo wa madeni ukikaribia jumla ya mapato ya kitaifa kwa mwaka.

Viwango vya maisha vimeshuka na huduma za umma zimedorora haswa Huduma ya Taifa ya Afya inayothaminiwa zaidi ambayo imezongwa na migomo ya kila mara.

Tayari Starmer amelazimika kusitisha, kwa muda baadhi ya mipango mikubwa ya chama cha Labour kama vile uwezekezaji katika miradi ya uzalishaji kawi safi na kutoongeza ushuru kwa “wafanyakazi”.

Uungwaji mkono kwa chama cha Conservative uliathiriwa zaii na chama cha Reform UK kinachoongozwa na Nigel Farage, aliyeongoza kampeni ya kushikiniza Uingereza ijiondoe kutoka Umoja wa Ulaya.

Farage alipinga sera za chama cha Conservative kuhusu uhamiaji.

Naye Starmer ameahidi kufutilia mbali sera tata ya Conservative ya kuwatuma wahamiaji nchini Rwanda.

Hata hivyo, atakabiliwa na presha ya kusaka suluhu ya kero la maelfu ya wahamiaji ambao huingia Uingereza kwa mashua.