Makala

Kwa akiba ya Sh50 kwa siku, wanachama 200 Kibra wamenunua matatu ya biashara

May 27th, 2024 2 min read

NA FRIDAH OKACHI

KWA miaka 16, wakazi mia mbili kutoka mtaa mabanda wa Kibra, Kaunti ya Nairobi walikusanya akiba zao kupitia chama ili kuinua viwango vyao vya maisha.

Wanachama hao wa muungano wa Egetureri ambao wengi wao ni wauza mboga, mahindi na wafanyakazi wa vibarua mbalimbali, walikuja pamoja ili kutatua masaibu wanayopata.

Mwenyekiti wa Muungano wa Egetureri Bw Ismail Maosa Sagana aliambia Taifa Dijitali kuwa jina Egetureri ni tarumbeta ambayo huleta watu kufanikisha jambo na kwa sauti moja.

Kupitia kwa chama hicho ambacho kilianza mwaka 2008, wanachama hao wameweza kununua ardhi nje ya Nairobi wakisubiri kupata pesa za ujenzi. Bw Sagana alisema kila mwanachama hutoa Sh50 kila siku.

“Wakati hatukuwa tunajuana wanachama waliogopa kutoa pesa zilizokuwa zikiwekwa na mmoja wetu. Lakini muda uliposonga tuliweza kufahamiana na kununua shamba nje ya Nairobi mwaka wa 2014,” alieleza.

Wanachama wa Egetureri, Kibra wakitabasamu kwa hatua waliyopiga. PICHA | FRIDAH OKACHI

“Tumenunua huko Ngong, Machakos na Kitengela. Wengi wetu hatujafanikiwa kujenga huko kwa kuwa bado tunakusanya pesa ili kila mmoja wetu aweze kuondoka kwenye maisha haya duni. Kuna wale ambao walikuwa na pesa. Hao wamefanikiwa kujenga na kuishi kwenye hizo ekari 80,” aliongeza.

Mwaka 2018, wanachama hao walianza kufanya mikutano ya mara kwa mara wakiwa na maono ya kununua gari ambalo lingetumika kama matatu. Bw Sagana alisema mradi huo ulikuwa mkubwa na ulihitaji mikakati kabambe.

“Tulitafuta watoaji mafunzo ya biashara ambao walikuja kutufahamisha jinsi ya kuwekeza. Kila siku tulikusanya Sh10,000 hadi mwaka 2023 tulipotafuta benki moja kutusaidia kununua gari la uchukuzi,” alifafanua Bw Sagana.

Wanachama hao wanasema wataendelea kuungana kwa pamoja ili kukamilisha kulipa mkopo huo.

Mwenyekiti wa chama cha Egetureri, Bw Ismail Sagana akiwa kando ya gari walilonunua. PICHA | FRIDAH OKACHI

“Kwa sasa gari linafanya kazi chini ya muungano wa Supermetro. Dereva na kondakta walifanyiwa mahojiano. Maono yetu kama chama tunatafuta kupata magari zaidi ya tano,” alisema.

Bw Ismail alisema mojawapo ya matatizo waliyokumbana na kuanzisha chama hicho ni changamoto ya fedha wakati wa kupatwa na msiba wa mara kwa mara kwenye mtaa huo.

“Tulikuwa tunakaa na marehemu zaidi ya wiki au mwezi kwa kuwa tumeshindwa ni wapi tutapata pesa za kusaidia waliofiwa,” alidokeza Bw Sagana.