Bambika

Muziki wa injili utazidi kudidimia Kenya sababu vibaraka wamejaa, Bahati adai


MSANII wa zamani wa injili na mshindi wa tuzo za Groove, Kevin Kioko almaarufu Bahati (Mtoto wa mama) amefunguka kuhusu kudidimia kwa muziki wa injili nchini katika miaka ya hivi karibuni.

Msanii huyo anasema Kenya itasalia kuwa ngome kuu ya wasanii wa injili japo kutakuwepo na changamoto ya kupata wasanii wakubwa kama ilivyokuwa miaka 10 iliyopita.

Kwenye mahojiano na Taifa Dijitali, Bahati anaeleza kuwa kibali hicho kinang’aa nchini Nigeria na Rwanda. Alitaja wasanii wa injili waliopewa kibali hicho walianza majivuno, chuki miongoni mwao na kusababisha kusambaratika.

“Kenya ilikuwa na itazidi kuwa ngome ya injili lakini sio kama miaka 10 iliyopita. Kwa sababu Mungu amehamisha kibali hicho…” Alisema Bahati.

Baba huyo alisema kuwa wingi wa vipaji vilivyokuwa vimekuzwa kanisani vimegeuzwa na kuwa na chuki.

“Si kwamba Kenya hatujui kuimba vizuri, au hatuna nyimbo nzuri za injili, hapana. Ukweli ni kwamba vipaji vimebadilishwa,” aliongeza Bahati.

Msanii huyo alisisitiza kwamba idadi kubwa ya vibaraka wamo kanisani ikilinganishwa na wale wapo kwenye muziki wa kidunia.

“Wakati mtu unafanikiwa, watu wanajumuika pamoja kwa haraka ili kukuangusha katika sekta ya injili kuliko sekta ya Gengetone,” alieleza.

“Sipendi kuzungumzia sana kuhusu masuala ya kanisa. Najua wanajijua watasema natafuta kiki lakini ukweli ni kwamba mimi huogopa sana kusongea sekta ya injili kwa kuwa najua jinsi wanachukiana,” alisema.

Hata hivyo mtoto wa mama alikiri kuwa yeye si mwokovu sana kuliko walio mtandaoni, akihimiza kila mmoja kuomba msamaha na kunyenyekea kwa Mungu.

“Kitu najua tunahitaji kuomba msamaha na kuacha kuwa vibaraka ili Mungu atupeleke katika kiwango kingine. Bila hivyo, mimi naomba Mungu aendelee kuinua Arbantone kwa kujifanya manaibu wa Yesu,” alikamilisha.

Bahati alianza kuvuma mwaka wa 2010 akiwa sekta ya injili, mwaka 2015 akaanza kufanya kolabo na wasanii wa sekula. Hadi ilipofikia mwaka 2023 na kujitokeza na kuweka wazi kuwa si msanii wa injili.