Maoni

TAHARIRI: Hekima ndiyo inahitajika nchini kurejesha utulivu

July 3rd, 2024 2 min read

KWA majuma kadha sasa, taifa la Kenya limejipata katika tandabelua kutokana na mkwaruzano wa kifalsafa kati ya umma na serikali ambao umeishia katika makabiliano na patashika, mali na maisha ya watu kupotea.

Ukizingatia matukio yote katika ukamilifu mzima, chanzo cha hali ya sasa kinaweza kuhusishwa na hatua ya viongozi walio mamlakani kuzinza vichwa na kutosikiliza rai za mamilioni ya raia.

Kwa muda mrefu, wananchi wamekuwa wakilalamikia hali ngumu ya maisha nchini kutokana na kupanda kwa bei ya bidhaa za msingi.

Licha ya kuwepo mfumko wa bei ya baadhi ya bidhaa kama vile mafuta kote duniani, nchini kwetu mengi ya masaibu wanayopitia wananchi yanatokana na athari za sera na maamuzi ya serikali iliyoko mamlakani.

Malalamishi kuhusu Mswada wa Fedha wa 2024 yalianzia katika majukwaa wazi miongoni mwa wanasiasa kisha mitandaoni miongoni mwa vijana na wataalamu.

Kadri muda ulivyopita, ilibainika wazi kwamba wananchi wengi walipinga ushuru mpya uliopendekezwa na mrengo wa Kenya Kwanza kupitia kwa Kamati ya Fedha na Mipango.

Baada ya shinikizo kuongezeka, Rais William Ruto aliongoza mrengo wa serikali na kupendekeza mabadiliko kadha ambayo kwa kweli yalileta nafuu.

Hata hivyo, vijana wa kizazi kipya waliokuwa wamekerwa na Mswada mzima wa Fedha walitaka wote mzima utupiliwe mbali.

Hatua ya Bunge la Kitaifa kupitisha Mswada huo iliwakera na kuwalazimu wajimwaye barabarani kuelezea ghadhabu zao.

Tangu siku hiyo kumekuwa na maandamano yaliyoishia katika kuvamiwa kwa bunge na hata sehemu ya bunge kuchomwa.

Kwingineko nchini, maandamano hayo yalisababisha uharibifu wa mali na watu kuangamia.

Baada ya matukio haya Rais William Ruto aliamua kukataa kuutia saini Mswada wa fedha na kuurejesha bungeni.

Hatua hii ilipoza joto nchini kiasi. Hata hivyo, hatua ya serikali kuendelea kuwanyaka watu mbalimbali kuhusiana na maandamano na uharibifu wa mali uliotokea imeendelea kukera wengi na hivyo kuchochea maandamano zaidi.

Mapendekezo zaidi yametolewa na vijana kwa serikali kama njia mojawapo ya kubadili mkondo wa gurudumu la uongozi wa taifa.

Inapendeza kwamba Rais amekubali baadhi ya mapendeezo yaliyotolewa na Rais ila bado wanashinikiza kiongozi wa taifa achukue hatua za dhati ili kuonesha kujitolea kwake.

Katika mvutano huu, ni lazima itajwe kwamba tofauti zetu kama taifa hazitasuluhishwa katika mazingira ya sasa.

Ipo haja kwa wahusika wote kulegeza msimamo ili kuwepo na mazungumzo ya dhati kurejesha utulivu.