Makala

TUONGEE KIUME: Mali ya mchumba kabla ya ndoa sio yako, labda uchangie kuiboresha


USIMEZEE mate mali ambayo mume au mkeo alipata kabla ya kuoana. Sheria  ya ndoa ya Kenya inasema mtu hawezi kudai umiliki wa mali ambayo mchumba wake alipata kabla ya kuoana.

Kwa hivyo, ukiangukia mume au mke mwenye mali, hauwezi ukadai ni yako.

Hata hivyo, unaweza kunufaika na mali hiyo kwa kuchangia kuiboresha na hivyo basi kudai sehemu yake. Hapa, wanaume wazembe hawana chao kwa kuwa kipengele hiki cha sheria kinapendelea wanawake.

Kwa upande mwingine, mali yoyote ambayo hupatikana wakati wa ndoa ambayo imesajiliwa kwa jina la mwanandoa mmoja, kuna dhana kwamba mali ya aina hiyo ni ya wanandoa wote wawili na aliyesajiliwa kama mmiliki anaishikilia kama amana kwa mke au mume wake.

Dhana hii inaweza kupingwa pale ambapo ushahidi unawasilishwa mbele ya mahakama kuthibitisha vinginevyo.

Ni kwa sababu hii kwamba idhini ya mchumba inahitajika kabla ya mali ya mtu yeyote aliyefunga ndoa kuhamishwa kwa kuuzwa  au kupeanwa kama zawadi, kukodishwa au kutumiwa kama dhamana ya mkopo.

Idhini hii inanuiwa kuhakikisha kuwa mume au mke anafahamu kuwepo kwa mali hiyo; kuwa mali hiyo imesajiliwa kwa jina la mchumba wao; anafahamu shughuli itakayofanyika na kwamba wamekubaliana nayo na anaelewa maana ya kutoa kibali kulingana na Sheria.

Licha ya maelezo yaliyo hapo juu, watu ndoa wanaweza pia kuchagua kuingia katika makubaliano ya kabla ya ndoa ili kusaidia kuamua haki zao za kumiliki mali.

Makubaliano kama haya ni halali. Hata hivyo mahakama inaweza kuyatupilia mbalik kwa misingi ya kulazimishwa au ulaghai au yakiwa yanakiunga sheria ya ndoa na umiliki wa mali.

Hivyo basi, kabla ya kuingia katika makubaliano kama haya, wahusika wanapaswa kushirikisha mawakili ili kupata ushauri wa kisheria wa kuhakikisha kwamba  ndoa ikivunjika mahakama inaweza kuzingatia na kutekeleza  makubaliano yao.

Makubaliano kama haya ni muhimu katika usimamizi wa mali mradi tu yawe yameandaliwa kwa haki na kuwe na uwazi na nia njema kutoka kwa wahusika.