Nasambu ahamia Uturuki kutoka Kayole
Mshambuliaji wa Kayole Starlets Calta Nasambu amejiunga na klabu ya Haymana Spor Kulübü inayoshiriki Ligi Kuu ya Soka la Wanawake nchini Uturuki.
Nasambu, 21, aliondoka nchini Jumatatu ilyopita kujiunga na klabu hiyo kwa mkataba utakaodumu hadi mwisho wa msimu Mei 2027, huku kukiwa na uwezekano wa kuongezwa kwa muda zaidi.
Mchezaji huyo anayeibukia aliwahi kuchezea Barcelona Ladies SC ya Laikipia kabla ya kujiunga na Kayole Starlets Februari mwaka huu. Aliisaidia Kayole kumaliza katika nafasi ya sita kwenye Ligi Kuu ya Wanawake nchini (KWPL) msimu uliopita.
Nasambu alisema kuhamia Uturuki ni kutimia kwa ndoto yake ya kucheza soka nje ya Kenya, akitambua mchango wa mashindano ya Safaricom Chapa Dimba katika kumfungulia milango ya fursa za kimataifa.
“Hii ni ndoto iliyotimia. Daima nimekuwa nikiomba kupata nafasi ya kucheza nje ya nchi na sasa ninaelekea Uturuki. Ninaamini huu ni mwanzo tu na nitajitahidi kupiga hatua zaidi katika taaluma yangu,” alisema Nasambu.
Aliongeza: “Safaricom iliponiwezesha kusafiri kwenda Uhispania kupitia Chapa Dimba, ilinifungulia milango ya fursa za kimataifa. Ninawashukuru sana. Pia ninaishukuru Barcelona Ladies SC na Kayole Starlets kwa kuniamini na kunipa nafasi ya kuonyesha kipaji changu.”
Akiwa Haymana Spor Kulübü, Nasambu ataungana tena na wachezaji wenzake wa zamani wa Kayole Starlets, Lavin Achola na Euphrasier Shilwatso, waliojiunga na klabu hiyo ya Uturuki Agosti mwaka huu.
Nasambu alivuma wakati wa msimu wa nne wa mashindano ya Safaricom Chapa Dimba alipokuwa akiichezea Barcelona Ladies SC. Aliibuka mfungaji bora wa mashindano hayo na kuisaidia timu yake kufuzu kwa fainali za kitaifa zilizofanyika Kisumu.
Kutokana na kiwango chake katika mashindano ya kanda na fainali za kitaifa, alichaguliwa kujiunga na kikosi cha Safaricom Chapa Dimba All-Stars kilichosafiri kwenda Huesca, Uhispania, mwaka 2025 kwa kambi ya mafunzo ya wiki moja.
Akiwa huko, Nasambu alipata nafasi ya kufanya mazoezi na kikosi cha kwanza cha wanawake cha Huesca baada ya kuvutia katika mechi za kirafiki zilizochezwa wakati wa ziara hiyo.
Mzaliwa wa Sikhendu, Kitale, Kaunti ya Trans Nzoia, Nasambu alikuza kipaji chake Barcelona Ladies SC chini ya kocha Emman Wafula Gullit kabla ya kuhamia Kayole Starlets.
Meneja wa Kayole Starlets, Faith Odit, alisema klabu hiyo inafurahia kuona mchezaji huyo akipata fursa ya kuendeleza taaluma yake nje ya nchi.
“Calta ni mmoja wa wachezaji wenye vipaji vikubwa katika Kayole Starlets. Uwezo wake wa kudhibiti na kumiliki mpira unaonyesha kuwa ana mustakabali mzuri. Tunafurahia kupata kwake nafasi ya kujiunga na Haymana Spor Kulübü kwa kipindi kilichosalia cha msimu na tunamtakia kila la heri,” alisema Odit.