Habari

Mahakama yaagiza mshukiwa wa pili katika mauaji ya mtangazaji azuiliwe kwa siku tisa

May 12th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na RICHARD MUNGUTI

MSHUKIWA wa pili katika mauaji ya mtangazaji wa kituo cha redio cha Pamoja FM amefikishwa kortini.

Juma Hussein Mohammed, mahakama iliamuru, azuiliwe kwa siku tisa kuhojiwa kuhusiana na mauaji ya Mohammed Hassan Marjan aliyeuawa akitoka kazini asubuhi ya Mei 4, 2020, katika mtaa Lindi, Kibra.

“Naomba hii mahakama iamuru mshukiwa azuiliwe kuhojiwa na kupelekwa kupimwa akili ibainike ikiwa ni timamu,” afisa anayechunguza mauaji hayo amemuambia hakimu mwandamizi Bernard Ochoi.

Hakimu mwandamizi Bernard Ochoi. Picha/ Richard Munguti

Juma alishikwa katika bustani ya Uhuru Park akijaribu kutoroka.

Juma atashtakiwa pamoja na Luqman Mohammed Ibrahim aliyeshikwa wiki iliyopita na kufikishwa kortini.

Akiwasilisha ombi la kuzuiliwa kwa Luqman afisa wa polisi Paul Mwachiro alimweleza hakimu mkazi Carolyne Muthoni Nzibe kuwa mshukiwa alitiwa nguvuni Jumatatu wiki jana na mahojiano yanaendelea.

Mwachiro alisema mshukiwa huyu anatazamiwa kuwasaidia polisi kuwasaka washukiwa wengine alioshirikiana nao kutekeleza uhalifu huo wakiwa wamejihami na silaha hatari.

Hakimu alifahanishwa mshukiwa anahitajika kupimwa akili ibainike ikiwa akili yake ni timamu kabla ya kufunguliwa mashtaka.

Bi Nzibo aliombwa aamuru mshukiwa azuiliwe siku 14.

Mahakama iliambiwa Marjan aliyekuwa na umri wa miaka 62 alishambuliwa na kundi la wanaume saba waliokutana naye katika eneo la Olimpiks akitoka kazini na wakamshambulia.

Alifariki baada ya muda mfupi.

Luqman atarudishwa tena mahakamani Mei 22, 2020, kwa maagizo zaidi.