Michezo

Klopp, Guardiola, Solskjaer na Ancelotti wataka EPL iruhusu klabu kuchezesha wanasoka watano wa akiba mechini

November 12th, 2020 Kusoma ni dakika: 3

Na MASHIRIKA

KOCHA Jurgen Klopp wa Liverpool ametaka vinara wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kufanyia mabadiliko ratiba ya kivumbi hicho akilalamikia kwamba ugumu wa mpangilio wa sasa ambao una mrundiko wa mechi unawaumiza wachezaji.

Kwa upande mwingine, mkufunzi Pep Guardiola wa Manchester City amesema kwamba wingi wa mechi zinazopigwa chini ya kipindi kifupi cha muda unachangia idadi kubwa ya majeraha mabaya ambayo yanatishia kulemaza uthabiti wa baadhi ya vikosi.

“Wachezaji hawapo salama. Wapo katika hatari ya kupata mejeraha yanayotishia taaluma yao na jambo hili litapunguza viwango vya ushindani na ubora wa ligi,” akasema Guardiola.

Kauli ya Guardiola imeungwa mkono na kocha Ole Gunnar Solskjaer wa Manchester United ambaye ametaka pia kubadilishwa kwa muda wa kupigwa kwa baadhi ya mechi kwenye ratiba ya EPL msimu huu.

“Ilikuwa vigumu kucheza dhidi ya Everton ugenini katika mechi ya mapema ya EPL mnamo Jumamosi iliyopita siku tatu pekee baada ya kuvaana na Istanbul Basaksehir kwenye gozi la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) ugenini,” akalalamika Solskjaer.

Liverpool na Man-City waliambulia sare ya 1-1 katika EPL mnamo Novemba 8, 2020 baada ya miamba hao wa soka ya Uingereza kusajili ushindi mnono kwenye michuano yao ya UEFA. Mohamed Salah alifunga bao la Liverpool kabla ya Gabriel Jesus kusawazisha.

“Wachezaji wana uchovu na hali hiyo ni hatari kwa usalama wao. Hakuna kikosi kilichocheza Novemba 4 kinastahili kupangwa tena kuwa uwanjani mapema Novemba 7. Heri Jumapili, lakini sis aa nane au saa tisa Jumamosi. Kufanya hivyo kunaumiza. Ina maana utakuwa ukilala na kuamkia uwanjani. Hakuna muda wa kutosha kupumzika,” akasema Klopp kwa kumuunga mkono Solskjaer.

Ingawa Man-United walisajili ushindi wa 3-1 dhidi ya Everton mnamo Novemba 7, Solskjaer ameshikilia kwamba waratibu wa gozi hilo lililopigiwa Goodison Park walikuwa na nia ya kushuhudia maanguko ya kikosi chake.

“Ilikuwa mechi ngumu ya ugenini iliyosakatwa saa chache baada ya safari ndefu ya kutoka Uturuki kwa gozi jingine kali la UEFA,” akasema kocha huyo raia wa Norway.

Guardiola amewataka vinara wa EPL kurejesha kanuni mpya ya kuruhusu jumla ya wachezaji watano wa akiba kuwajibishwa katika mchuano mmoja.

“Zaidi ya asilimia 47 ya mejaraha yanayouguzwa na wanasoka wa klabu mbalimbali ni ya misuli. Ina maana kwamba tatizo ni la kuchezeshwa sana uwanjani bila ya kupata muda wa kupumzika vya kutosha,” akasema kocha huyo wa zamani wa Barcelona na Bayern Munich.

Vikosi vingi vya EPL vilipiga kura ya kukataa kuidhinishwa kwa kanuni hiyo ya kuchezeshwa kwa wanasoka watano wa akiba katika mechi moja msimu huu wa 2020-21.

Sheria hiyo ilipendekezwa na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) ilianza kutekelezwa wakati soka ya EPL iliporejelewa mnamo Juni 2020 baada ya kusitishwa kwa zaidi ya miezi mitatu kutokana na janga la corona.

Katika msimu huu, EPL ilirejelea mfumo wa zamani unaoruhusu kila kikosi kufanya hadi mabadiliko matatu pekee katika mchuano mmoja.

Kuhusu haja ya kupunguzwa kwa idadi ya wanasoka wa akiba walio na uwezo wa kuwajibishwa katika mechi moja, vikosi vingine vilihisi kwamba klabu ‘kubwa’ zilikuwa katika hali bora na uwezekano mkubwa zaidi wa kunufaika katika mechi licha ya kanuni hiyo kudumishwa na FIFA na kusalia maamuzi ya klabu za ligi mbalimbali kuamua iwapo zitaendelea kuitekeleza au la.

FIFA ilisisitiza kwamba wachezaji watano wa akiba wanaweza kuchezeshwa katika mechi moja katika mapambano ya hadi Agosti 2021, kumaanisha kwamba kanuni hiyo ipo huru kutumika katika fainali zijazo za Euro na Copa America.

Vikosi vya EPL pia vilipitisha kura ya kuendelea kupangwa kwa wachezaji saba pekee kwenye kikosi cha akiba cha kila timu wakati wa mechi.

Man-City na Liverpool ni miongoni mwa vikosi vya EPL ambavyo vimelemazwa zaidi na wingi wa visa vya majeraha.

Huku Man-City wakilazimika kukosa huduma za Sergio Aguero, Benjamin Mendy na Nathan Ake kwa muda mrefu, Liverpool wataendelea pia kukosa maarifa ya wachezaji Fabinho na Virgil va Dijk. Wawili hao wanaingia mkekani baada ya beki Joel Matip na kipa Alisson Becker kupona.

Maoni ya Guardiola yameungwa mkono na Solskjaer, Frank Lampard wa Chelsea na Carlo Ancelotti wa Everton.