Junior Starlets kaunza kazi ya Kombe la Dunia U17 dhidi ya China
Timu ya taifa ya soka ya mabinti wasiozidi miaka 17, Junior Starlets, itaanza kampeni yake ya Kombe la Dunia kwa kuvaana na China leo, kuanzia saa moja jioni saa za Kenya, katika uwanja wa Akademia ya Mohammed VI Football mjini Salé, kaskazini-magharibi mwa Morocco.
Mashindano hayo yanayoshirikisha mataifa 24 yalianza Jumamosi iliyopita na yataendelea hadi Novemba 7.
Mwenyeji Morocco alianza kwa ushindi wa 4-0 dhidi ya New Zealand, huku mabingwa watetezi Korea Kaskazini wakiilaza Puerto Rico. Ujerumani iliishinda Argentina 2-1, sawa na Poland iliyozidiwa Nigeria kwa matokeo kama hayo.
Chini ya kocha Mildred Cheche, Junior Starlets iliwasili Morocco Oktoba 8 na kujiandaa kwa ushindi wa mabao 23-0 dhidi ya Raja Casablanca Women kabla ya kupoteza 2-1 dhidi ya Ghana. Mshambuliaji Brenda Achieng’ ndiye aliyefunga bao la Kenya dhidi ya Ghana.
Cheche alisema mechi hizo za kirafiki ziliwasaidia kutambua maeneo yanayohitaji kuboreshwa, hasa kufunga mabao.
Kikosi hicho cha wachezaji 21 kinajumuisha kiungo Peninah Fostine na mshambuliaji Joan Agola wa pamoja na mshambuliaji Mwanakombo Bakari, aliyejiunga na timu hiyo akitokea Marekani.
Hata hivyo, mshambuliaji Faith Boke wa Shule ya Upili ya Wasichana ya Butere, hakujumuishwa kwenye kikosi chamwisho kutoka na jeraha ingawa alisafiri na timu. Wengine walioachwa nje ni beki Idah Matara, kiungo Clarice Demba na mshambuliaji Patience Waithira.
Baada ya mechi ya leo, Kenya itakutana na Marekani Alhamisi hii kabla ya kumalizana na Samoa Oktoba 25. Mechi zote zitachezwa katika uwanja huo huo wa Mohammed VI.
Starlets ilifuzu kwa mashindano hayo baada ya kuishinda Namibia kwa jumla ya mabao 7-1, kuiondoa Uganda kwa bao la ugenini baada ya sare ya 1-1, kisha kuilaza Afrika Kusini kwa jumla ya mabao 5-1.
Wakishiriki Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza 2024 nchini Jamhuri ya Dominican, Kenya ilimaliza ya tatu katika Kundi C ikiwa na alama tatu. Ilipoteza dhidi ya Uingereza (2-0) na Korea Kaskazini (3-0), lakini ikaishinda Mexico 2-1.
Kenya ilikosa mashindano ya mwaka jana baada ya kuondolewa na Cameroon kwa jumla ya mabao 4-1 katika mechi ya raundi ya mwisho ya kufuzu.
Cheche amesema lengo lao safari hii ni kufuzu kwa hatua ya 16 bora badala ya kushiriki tu.
China, ambayo inafundishwa na Wang Hongliang tangu 2023, inashiriki Kombe la Dunia kwa mara ya nne. Katika mashindano ya mwaka jana nchini Morocco, ilifika hatua ya 16 bora kabla ya kuondolewa na Brazil kwa kichapo cha mabao 3-0.
Mechi ya leo itakuwa ya kwanza kati ya Kenya na China.