Talanta kuandaa mashindano ya HSBC SVNS 2 mwaka 2027
Uwanja wa Talanta jijini Nairobi utakuwa mwenyeji wa mashindano ya raga ya HSBC SVNS 2 mnamo Januari 23 na 24, 2027, baada ya Shirikisho la Raga Duniani kuthibitisha kuwa Kenya itakuwa mwenyeji kwa mwaka wa pili mfululizo.
Nairobi itaandaa awamu ya kwanza ya mashindano hayo ya kimataifa ya raga ya wachezaji saba kila upande (wanawake kwa wanaume), kabla ya msururu huo kuelekwa Montevideo, Uruguay, Februari 20 na 21, kisha Sao Paulo, Brazil, Februari 27 na 28.
Miji hiyo mitatu imerejea kama wenyeji baada ya kuandaa mashindano ya kwanza ya HSBC SVNS 2 mwaka huu, hatua inayolenga kupanua ,mchezo wa raga ya wachezaji saba katika mataifa yanayoibukia katika mchezo huo.
Meneja Mkuu wa Shirikisho la Raga Duniani, Sam Pinder, alisema mashindano hayo yatazipa timu nafasi nyingine ya kupigania kupanda daraja hadi kiwango cha juu cha raga ya kimataifa.
“Tunafurahia kuthibitisha kurejea kwa Nairobi, Montevideo na Sao Paulo kwa mashindano ya HSBC SVNS 2 mwaka 2027. Mashindano ya msimu uliopita yalidhihirisha umuhimu wa jukwaa hili katika kuzipa timu njia ya wazi na yenye ushindani mkali ya kufuzu kwa dunia ya HSBC SVNS,” alisema Pinder.
Aliongeza kuwa maandalizi ya kufuzu kwa Michezo ya Olimpiki ya Los Angeles 2028 yanaongeza umuhimu wa kila hatua ya mashindano hayo.
Mfumo wa HSBC SVNS una madaraja matatu yanayounganisha mashindano ya kufuzu katika kanda mbalimbali, HSBC SVNS 3, HSBC SVNS 2 na HSBC SVNS ambayo ni mashindano ya Kombe la Dunia.
Kwa upande wake, Afisa Mkuu Mtendaji wa Chama cha Raga nchini (KRU), Thomas Odundo, alikaribisha uteuzi wa Nairobi, akisema chama hicho kimejipanga kuandaa mashindano mengine yenye mafanikio.
Uteuzi huo unafuatia kuandaliwa kwa mashindano ya 28 ya Safari 7s katika Uwanja wa Nyayo jijini Nairobi, ambaye yalikamilika siku chache zilizopita.
Katika mashindano ya HSBC SVNS 2 yaliyofanyika Nairobi mwaka huu, Ujerumani ilitwaa taji la wanaume huku Argentina ikishinda taji la wanawake.
Mashindano ya mwaka ujao yatazipa timu za Kenya za wanaume na wanawake fursa nyingine ya kupimana nguvu na wapinzani wa kimataifa huku zikilenga kupiga hatua katika mfumo wa kimataifa wa raga ya wachezaji saba kila upende.