Hofu Garissa baada ya mwanamume kulazimishwa kumeza msumari
WAKAZI wa Garissa wanaishi kwa hofu kufuatia ongezeko la mashambulizi ya magenge, huku mwanamume mmoja akilazimishwa kumeza msumari wa urefu wa inchi nne ili asikatwe kwa mapanga.
Daniel Musyoka, 38, mfanyakazi wa vibarua, alisema alishambuliwa mnamo Oktoba 26 alipokuwa akirejea nyumbani kutoka kazini eneo la Madogo, Kaunti ya Tana River.
Alisimulia kuwa wanaume wanne waliokuwa wameficha nyuso zao walimnyang’anya Sh420 na sigara nne, kabla ya kutaka pesa zaidi.
Mmoja wao alimpa msumari na kumtaka achague kuumeza au kukatwa vipande kwa mapanga.
Musyoka alimeza msumari huo akihofia maisha yake. Siku nne baadaye alifika Hospitali ya Rufaa ya Garissa ambako eksirei ilionyesha msumari ulikuwa umesafiri karibu mfumo mzima wa chakula.
Daktari Naibei Abdon alisema msumari ulikuwa kwenye utumbo mpana na mgonjwa hakuwa hatarini, hivyo madaktari walikuwa wakifuatilia hali yake bila ya upasuaji.
Wakati huo huo, Amos Aura amelazwa hospitalini akiwa amevunjika mguu baada ya kushambuliwa na vijana waliomnyang’anya simu na pesa.
Anahitaji Sh40,000 kufanyiwa upasuaji.
Hofu imeongezeka pia baada ya mwili wa mwendesha bodaboda Jackson Wambua, 24, kupatikana Modika siku tano baada ya kutoweka.
Polisi wanachunguza mauaji yake na wanasema pikipiki yake iliibwa.
Polisi wanasema uchunguzi unaendelea kubaini waliohusika na mashambulizi hayo na kukabiliana na magenge yanayotishia usalama wa wakazi.