Waziri Joho arejea shuleni, aendea digrii ya uzamili na kupuuzilia mbali kejeli za D-
WAZIRI wa Madini, Uchumi wa Bahari na Masuala ya Ubaharia, Bw Hassan Joho, ametoa changamoto kwa vijana wajitahidi maishani, huku ikifichuka kwamba anaendeleza masomo ya uzamili katika Chuo Kikuu cha Kiufundi cha Mombasa (TUM).
Naibu Chansela wa chuo hicho, Profesa Laila Abubakar, alithibitisha Bw Joho ni mwanafunzi katika chuo hicho licha ya majukumu yake mazito katika Baraza la Mawaziri.
Duru katika chuo hicho zilisema anasomea shahada ya uzamili katika Masomo ya Maendeleo, akiwa anakamilisha mwaka wake wa kwanza huku mitihani ikiendelea. Kozi hiyo huchukua miaka miwili.
Kwa miaka mingi, Bw Joho amekuwa akikejeliwa kwa kupata alama ya D- kwenye mtihani wake wa kitaifa wa kidato cha nne (KCSE).
Hata hivyo, amekuwa akieleza safari yake kama ushahidi wa uvumilivu, akitaja umaskini na changamoto za kifedha alizokabiliana nazo akiwa kijana kuwa sababu kuu zilizochelewesha masomo yake.
Akizungumza chuoni humo Jumanne, Bw Joho alitafakari kuhusu gharama ya kupoteza muda na vikwazo vya kimuundo vinavyowakabili vijana kutoka familia zisizojiweza.
“Muda unaweza kuwa na gharama kubwa kwa baadhi ya watu, kiasi cha kubadilisha maisha yao kabisa. Niulizeni mimi, mtu ambaye alipata fursa ya kuendelea na elimu ya juu akiwa mtu mzima,” alisema Bw Joho.
Alieleza jinsi umaskini unavyowalazimu vijana wengi kufanya kazi kabla ya kuendelea na masomo, akisimulia masaibu yake mwenyewe alipokuwa shule ya upili ambapo alilazimika kusawazisha kazi na masomo.
“Nilifanya kazi nilipokuwa shule ya upili. Kwa kweli, siku nitakapoandika kitabu changu, nitaeleza kisa hicho kwa undani. Nilikuwa na makubaliano mazuri na mkuu wa shule. Nilimwambia ‘bwana, usijisumbue kunihusu, usinifukuze’ kwa sababu bado nilikuwa nikiondoka shuleni mapema tofauti na wanafunzi wengine. Kwa nini? Kwa sababu nilihitaji kufanya kazi kujiongezea kipato,” alifichua.
Aliwahimiza vijana kushiriki katika siasa bora ili kusaidia kuunda sera zitakazowalinda vizazi vijavyo dhidi ya changamoto kama hizo.
Wakati wa kuhojiwa na Kamati ya Bunge la Kitaifa ya Uteuzi mwaka 2024 kuhusu uteuzi wake katika Baraza la Mawaziri, Bw Joho alizungumzia kwa uwazi historia yake ya elimu mbele ya jopo lililoongozwa na Spika wa Bunge Moses Wetang’ula.
Aliwaambia wabunge kuwa alipata alama ya D- (minus) katika KCSE mwaka wa 1993 katika Shule ya Upili ya Serani, akieleza kuwa changamoto za kijamii na kiuchumi zilimwathiri kielimu.
Baada ya mitihani yake ya KCSE mwaka 1993, changamoto za kifedha zilimlazimu Bw Joho kuchelewesha kujiunga na masomo ya baada ya sekondari. Baadaye alifuata mkondo rasmi wa elimu, akihitimu kozi ya cheti katika usimamizi wa biashara mwaka 2008 na diploma ya usimamizi wa rasilimali watu mwaka 2007.
Baadaye alipata Shahada ya Usimamizi wa Biashara kutoka Chuo Kikuu cha Kampala mwaka wa 2013 na shahada ya pili kutoka Gretsa University mjini Thika.
Kabla ya kujiunga na TUM, Bw Joho pia alisomea uongozi wa umma katika Harvard Kennedy School of Government.
Akizungumzia maswali ya mara kwa mara kuhusu vyeti vyake vya elimu wakati wa kuhudumu kama Mbunge wa Kisauni (2007–2013) na Gavana wa Mombasa (2013–2022), Bw Joho alisema viongozi hushukiwa bila haki, akisisitiza kuwa njia zisizo za kawaida za kupata elimu zinaweza pia kutoa viongozi waliohitimu kikamilifu.