Habari za Kitaifa

Kindiki, Mudavadi washtakiwa kugawa mamilioni kwenye mikutano

Na JOSEPH WANGUI November 5th, 2026 Kusoma ni dakika: 1

NAIBU wa Rais Kithure Kindiki, Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi na viongozi wengine wa serikali wamefikishwa kortini kuhusiana na mamilioni ya pesa wanayotoa katika hafla tofauti nchini.

Katika kesi yake, mlalamishi Kelvin Kipchirchir anataka Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) ichunguze chanzo cha fedha na mali wanayogawa kwa wananchi.

Bw Kipchirchir anadai viongozi hao wamekuwa wakigawa pesa, magari, pikipiki na bidhaa nyingine katika hafla za uwezeshaji bila kuwa sehemu ya mipango rasmi ya serikali.

Anataka Mahakama Kuu kuagiza EACC ichunguze chanzo cha utajiri huo na kubaini iwapo viongozi hao walikiuka sheria za maadili na matumizi ya rasilimali za umma.

Kesi hiyo iliyowasilishwa Julai 31, 2025, ilitajwa Jumatano mbele ya Jaji Roselyne Aburili, lakini haikuendelea baada ya Kipchirchir kukosa kufika mahakamani.

Mawakili wa serikali na wa Bunge waliomba kesi hiyo itupiliwe mbali. Jaji Aburili alisema mahakama haitatupilia mbali kesi ambayo wahusika tayari wamewasilisha hoja zao kwa maandishi.

Kipchirchir anadai Kindiki amegawa zaidi ya Sh1 bilioni, huku Mbunge Oscar Sudi akidaiwa kutoa Sh145 milioni kupitia pesa taslamu na bidhaa.

Viongozi wengine waliotajwa ni Spika wa Bunge Moses Wetang’ula, Kiongozi wa Wengi Kimani Ichung’wah, msaidizi wa Rais Farouk Kibet, wabunge Didmus Barasa na Silvanus Osoro, pamoja na Seneta wa Kericho Aaron Cheruiyot.

Mlalamishi anasema fedha hizo hazikutengewa bajeti wala kutangazwa kama miradi rasmi ya serikali.

Anadai baadhi ya hafla hizo zilitumia majukwaa na rasilimali za umma na huenda zikawa njia ya kuwashawishi wapiga kura.

Anataka mahakama izuie viongozi hao kugawa mali nje ya mipango iliyoidhinishwa na kuagiza EACC ichunguze chanzo cha fedha hizo.

Kesi itatajwa Januari 19, 2027, kuweka tarehe ya uamuzi kutolewa.