Habari za Kitaifa

Maelfu wakimbilia Moyale mapigano yakichacha Ethiopia

Na DAVID MUCHUI October 23rd, 2026 Kusoma ni dakika: 2

Hali ya wasiwasi imetanda mjini Moyale, kaunti ya Marsabit, huku maelfu ya wanawake na watoto wakikimbilia Kenya kutafuta usalama kufuatia mapigano makali kati ya vikosi vya Somali na Oromia nchini Ethiopia.

Mapigano kati ya vikosi vya maeneo ya Nne na Tano nchini humo pamoja na maafisa wa usalama yameingia siku ya nne, huku milio ya risasi ikisikika karibu na mpaka.

Wakazi walisema mapigano yaliripotiwa Ijumaa asubuhi katika maeneo ya Moyale na Hudhat nchini Ethiopia.

Maelfu ya waliokimbia makazi yao wameingia Kenya, baadhi wakitafuta hifadhi kwa jamaa zao huku wengine wakilala mitaani na katika maeneo ya umma. Mamia wamepata hifadhi katika madrasa ya Manyatta, wadi ya Heillu Manyatta.

Ali Abdullahi, mkazi wa Moyale, alisema mapigano yalikuwa yakiendelea takriban kilomita tano kutoka upande wa Kenya.

“Mnamo Alhamisi, risasi  ziliwapata baadhi ya watu na majengo upande wa Kenya. Wakenya kadhaa walijeruhiwa na tuna hofu kuwa mapigano haya yanaweza kuendelea,” alisema.

Mfanyabiashara Ali Mumin alisema biashara kadhaa, zikiwemo benki, zimefungwa kutokana na hali ya usalama.

“Biashara zimeathirika pakubwa kwa sababu tunategemea sana biashara kutoka Ethiopia. Kufikia sasa, maelfu ya wakimbizi wamekimbilia maeneo mbalimbali mjini Moyale,” alisema.

Kamishna wa Kaunti ya Marsabit, Stanley Kamande, alisema maafisa wa usalama wanafuatilia hali hiyo kuzuia mapigano yasivuke mpaka.

Aliwataka wakazi kuwa macho na kuripoti shughuli zozote zinazotiliwa shaka, huku akiomba mashirika ya kibinadamu kusaidia wakimbizi.

Katibu Mkuu wa Shirika la Msalaba Mwekundu Kenya, Ahmed Idris, alisema shirika hilo limeanza kusaidia familia zilizoingia nchini, likilenga awali 1,000.

Alisema wengi waliwasili bila mali nyingi na wanahitaji haraka makazi, chakula, maji na huduma za afya.

Wahudumu wa shirika hilo, kwa ushirikiano na serikali ya kaunti ya Marsabit na maafisa wa serikali ya kitaifa, walitoa mahema, blanketi, mikeka, mitungi ya maji na vifaa vya jikoni.

Pia wanatoa huduma ya kwanza na chakula maalumu chenye virutubisho kwa watoto wadogo na kina mama wajawazito na wanaonyonyesha.

Shirika hilo pia linasaidia familia zilizotenganishwa na mapigano kuwasiliana tena.

“Kipaumbele chetu ni kuhakikisha kila familia inayowasili Moyale iko salama, ina makazi na inatendewa utu,” alisema Dkt Idris.