Sababu za wadau wa elimu kupinga mageuzi ya Ruto
WADAU wakuu katika sekta ya elimu wamepinga miswada saba ya mageuzi ya elimu inayosukumwa na Rais William Ruto, wakisema inaweza kufuta mafanikio yaliyopatikana iwapo haitafanyiwa marekebisho.
Miswada hiyo, ambayo iko katika hatua ya kukusanya maoni ya umma kupitia Kamati ya Elimu ya Bunge la Kitaifa, inalenga kubadilisha usimamizi wa shule, mafunzo ya walimu, ufadhili wa wanafunzi na uteuzi wa nafasi katika vyuo vikuu na taasisi za kiufundi.
Vyama vya walimu, wahadhiri, wazazi na wamiliki wa shule za kibinafsi wamewasilisha mapendekezo yao, wakishinikiza wabunge kuyazingatia kabla ya kupitisha sheria hizo.
Chama cha Wahadhiri wa Vyuo Vikuu (UASU) kinataka sheria inayopendekezwa kuhusu ufadhili wa elimu ya juu ilinde wanafunzi ambao tayari wanapokea mikopo na ufadhili wa masomo, pamoja na haki za wafanyakazi wa vyuo vikuu.
Chama hicho pia kinataka serikali kufanya tathmini ya gharama za utekelezaji wa mfumo huo kabla ya kuanza kutumika.
Kinasema mswada huo unaangazia zaidi ufadhili wa wanafunzi huku ukipuuza gharama ya kuendesha vyuo vikuu na kulipa wahadhiri.
UASU pia inapinga sharti linalotaka wahitimu kuanza kurejesha mikopo ndani ya mwaka mmoja baada ya kumaliza masomo. Inataka muda huo uanze tu baada ya mhitimu kupata kazi yenye mapato ya uhakika.
Chama hicho kinataka pia kuwakilishwa katika bodi za Mamlaka ya Ufadhili wa Elimu ya Juu na Huduma ya Kitaifa ya Uteuzi wa Wanafunzi wa Vyuo Vikuu na Vyuo vya Kiufundi (KUCCPS).
Chama cha Walimu wa Shule za Upili na Vyuo vya Kati (KUPPET) pia kimepinga muda wa mwaka mmoja wa kuanza kulipa mikopo, kikisema ni mgumu kwa wahitimu katika soko la ajira lenye ushindani.
Kinataka ufadhili huo uwe na chanzo cha wazi cha fedha na kiwango kisichozidi asilimia 2.5 ya mapato ya kila mwaka ya ushuru yanayokusanywa na Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru (KRA).
KUPPET pia inataka serikali itoe ufadhili kupitia ruzuku, ufadhili wa masomo na mikopo kulingana na mahitaji ya wanafunzi.
Chama cha Wakufunzi wa Vyuo vya Kiufundi na Mafunzo ya Ufundi (KUTVET) kinasema mfumo unaopendekezwa hauzingatii tofauti za gharama za kozi mbalimbali.
Kinasema kozi kama uhandisi wa magari, uchomeleaji, umeme na ujenzi zinahitaji vifaa na mafunzo ya vitendo ambayo hayawezi kugharimiwa kwa kiwango sawa na kozi zinazofundishwa darasani pekee.
Chama hicho kinataka fedha zitumike pia kununua mashine, vifaa vya usalama, teknolojia za kisasa na kugharamia mafunzo ya vitendo viwandani.
Wakati huo huo, Chama cha Walimu wa Shule za Msingi (KNUT) kimepinga pendekezo linalotaka walimu kutoshiriki shughuli nyingine za kujipatia mapato wanapohudumu katika Tume ya Huduma za Walimu (TSC).
KNUT kinasema tume hiyo haipaswi kudhibiti shughuli za walimu nje ya saa rasmi za kazi.
Kwa upande wake, Chama cha Shule za Kibinafsi nchini kinataka sheria itambue shule za Sekondari Msingi zinazojitegemea, badala ya kuzilazimisha kuwa na sehemu ya shule za msingi za kawaida.
Pia kinataka wanafunzi wa shule za kibinafsi waruhusiwe kunufaika na ufadhili wa masomo na basari za serikali bila kubaguliwa kwa sababu tu wanasomea katika taasisi hizo.
Chama cha Kitaifa cha Wazazi kinataka wazazi wapewe nafasi kubwa zaidi katika maamuzi ya elimu kupitia marekebisho ya sheria ya elimu ya msingi.
Wadau hao wanataka maoni yao yazingatiwe kabla ya miswada hiyo kuwasilishwa bungeni kwa hatua zaidi. Kamati ya Bunge inatarajiwa kukamilisha zoezi la kupokea maoni Alhamisi ijayo, baada ya kusikiliza TSC na Baraza la Magavana.