Habari za Kitaifa

Wabunge wambana Murkomen wakimlaumu kushindwa kudhibiti uhuni na utekaji nyara

Na SAMWEL OWINO November 6th, 2026 Kusoma ni dakika: 2

WAZIRI wa Usalama wa Ndani Kipchumba Murkomen alikabiliwa na maswali mazito kutoka kwa wabunge kuhusu ongezeko la visa vya utekaji nyara na uhuni kabla ya uchaguzi mkuu ujao.

Alipofika mbele ya bunge kujibu maswali, wabunge walimshutumu Waziri kwa kutojitahidi vya kutosha kudhibiti utamaduni wa uhuni unaoshamiri katika mikutano mingi ya kisiasa na kukosa kujibu kuhusu watu walioripotiwa kutoweka.

Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula alisimulia jinsi nusura afe alipohudhuria mazishi ya mamake mbunge wa Nyando, Jared Okelo katika Kaunti ya Kisumu.

“Nilikwenda kwenye mazishi ya mama ya mmoja wa wabunge mjini Nyando. Nusura nipoteze maisha yangu kwa wahuni,” alisema Bw Wetang’ula said.

Mbunge wa Suba Kaskazini Millie Odhiambo alionya kuwa endapo serikali itakosa kuzima utamaduni wa uhuni, kuna hatari ya vifo zaidi kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2027.

“Nina wasiwasi kwamba hatukabiliani na suala hili la uhuni ipasavyo na litatuathiri kama taifa,” alisema Bi Odhiambo.

“Ikiwa hatutachukulia hili kwa uzito, tutakuwa na vifo vingi. Sijali ni kambi ipi ya kisiasa, sehemu kubwa inachochewa nasi wanasiasa, kamata wanasiasa ikiwemo wabunge na uwashtaki,” alisema.

Mbunge wa Embakasi Magharibi Mark Mwenje alisema uchaguzi wa amani 2027 unategemea jinsi serikali itakavyokabiliana na uhuni.

“Tunataka Waziri atuhakikishie kuwa atakabiliana na masuala haya bila kujali ikiwa wahusika wako serikalini au upinzani. Nawahakikishia, akikabiliana na masuala haya, tutakuwa na chaguzi za amani,” alisema Bw Mwenje.

Kiongozi wa Wengi Kimani Ichung’wah alishutumu Waziri kwa kukosa kukabiliana na waliokiri kupanga wahuni, akirejelea matamshi aliyotoa majuzi aliyekuwa mbunge wa Makadara Reuben Ndolo.

“Ndolo alithibitisha kwenye televisheni kuwa alipanga wahuni na polisi wako hawakufanya lolote. Ni sharti tuchukulie kwa uzito zaidi jambo hili la uhuni kwa sababu ni sisi wanasiasa ndio huchochea maswala hayo,” alisema Bw Ichung’wah.

Bw Ndolo alijigamba katika kanisa la Jesus Teaching Ministry, Donholm, Oktoba 18 2026, kwamba aliwasafirisha vijana katika mikutano mbalimbali ya kisiasa, ikiwemo ukumbusho wa aliyekuwa waziri mkuu Raila Odinga katika uwanja wa Migwena, Bondo, Kaunti ya Siaya.

Bw Murkomen aliwaeleza wabunge kuwa hakuna kitengo cha polisi wala maafisa wanaoruhusiwa kumteka nyara yeyote akihakishia bunge kwamba visa vinachunguzwa.

Alisema wahuni zaidi ya 100 walikamatwa kuhusiana na tukio lililofanyika Homa Bay wakati wa mkutano wa Linda Mwananchi na kuwasilishwa katika korti mbalimbali.

Mbunge wa Mandera Kusini pia alieleza kuwa familia ya afisa wa akiba wa polisi Ali Issack Abdullahi imekuwa ikisubiri majibu kwa miezi miwili tangu alipotoweka.

Akijibu maswali hayo, Bw Murkomen alisema uchunguzi unaendelea na polisi wanafuatilia taarifa zote ili kubaini waliko watu waliotoweka na kuwakamata waliohusika.

Alisisitiza kuwa hakuna kitengo cha polisi wala afisa aliyeidhinishwa kumteka mtu yeyote.

Mark Mwenje alisema hatua kali dhidi ya wahuni bila kujali misimamo yao ya kisiasa ndiyo itakayowezesha uchaguzi wa amani mwaka 2027.