HabariHabari za Kitaifa

Ilikuwa utani tu – Hassan Omar ajitetea kuhusu ‘wafu kupiga kura’

Na NDUBI MOTURI October 22nd, 2026 Kusoma ni dakika: 2

KATIBU Mkuu wa chama cha UDA Hassan Omar ameitaka Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kutupilia mbali malalamishi dhidi yake kuhusu kauli aliyotoa kuwa hata watu waliokufa wanaweza kupiga kura katika uchaguzi mkuu wa 2027.

Omar alisema matamshi hayo aliyotoa Septemba 11 yalikuwa mzaha wa kisiasa uliolenga kuwahamasisha wakazi wa Pwani kujisajili kama wapigakura na kushiriki uchaguzi, wala si wito wa kufanya udanganyifu.

Alisema hayo Jumatano  akijitetea mbele ya kamati ya IEBC inayoshughulikia ukiukaji wa kanuni za maadili ya uchaguzi katika majengo ya Anniversary Towers, Nairobi.

Kupitia mawakili wake Emmanuel Kibet na Adrian Kamotho, Omar aliomba kamati imwachilie huru kwa madai kuwa hakuna ushahidi wa kutosha kuthibitisha kuwa alikiuka kanuni hizo. Hata hivyo, aliomba apewe onyo iwapo atapatikana na hatia.

Kibet alisema kauli hiyo ilipaswa kutathminiwa katika muktadha wa hotuba nzima, akisisitiza kuwa Omar alikuwa akiwahimiza wananchi walio na haki ya kupiga kura kujisajili na kuthibitisha taarifa zao kwenye sajili ya wapigakura.

“Ni wazi kuwa wakazi wa Pwani hawajajisajili kama wapigakura kwa wingi. Tunaamini kauli yake inapaswa kuangaliwa katika muktadha wake ili maana halisi ijitokeze,” alisema Kibet.

Omar alieleza kuwa Mombasa ilikuwa imesajili wapigakura wapya 12,000 hadi 13,000 pekee, licha ya kuwa na takriban watu 200,000 wanaostahili kujisajili.

Alisema juhudi zake za kisiasa zimekuwa zikilenga kukabiliana na kutengwa kwa wakazi wa Pwani, akitaja changamoto za kupata vitambulisho na kutambuliwa kama raia.

Omar alisisitiza kuwa wanasiasa hutumia tashbihi na kutia chumvi katika hotuba zao ili kufikisha ujumbe, na kwamba matamshi yake hayakupaswa kuchukuliwa kihalisi.

Hata hivyo, makamishna wa IEBC walionya kuwa kauli zinazohusisha matumizi ya majina au alama za vidole za watu waliokufa kupiga kura zinaweza kuibua wasiwasi kuhusu uadilifu wa uchaguzi.

Mwenyekiti wa kamati, Moses Alutalala Mukhwana, alikanusha madai kuwa IEBC inalenga viongozi wa UDA pekee, akisema kuitwa kwa maafisa kadhaa wa chama hicho mbele ya kamati hakumaanishi kuwa kuna ubaguzi.

Alihimiza vyama kuwasilisha malalamishi yao kupitia Kamati ya Ushirikiano wa Vyama vya Kisiasa badala ya kutumia makosa yanayodaiwa kufanywa na wapinzani kuhalalisha mienendo yao.

Kamati hiyo inatarajiwa kutoa uamuzi wake Oktoba 27.