HabariHabari za Kitaifa

Mashirika yashtaki kutaka ghasia za uchaguzi zizuiwe kabla ya 2027

Na SAM KIPLAGAT October 29th, 2026 Kusoma ni dakika: 2

MASHIRIKA matatu ya kutetea haki za binadamu yamewasilisha kesi katika Mahakama Kuu yakitaka serikali iunde jopokazi la mashirika mbalimbali ndani ya siku 30 kuchunguza na kuwafungulia mashtaka wanaohusika na ghasia za kisiasa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2027.

Mashirika hayo ni Kenya Human Rights Commission (KHRC), Katiba Institute na Independent Medico-Legal Unit (IMLU).

Yanasema kutoshughulikiwa kwa mashambulizi dhidi ya watu wanaoshiriki shughuli za kisiasa na kijamii kunatishia uhuru wa kikatiba na uadilifu wa uchaguzi.

Kesi hiyo inataja Mwanasheria Mkuu Dorcas Oduor, Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Ujasusi Noordin Haji, Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja na Waziri wa Usalama wa Ndani Kipchumba Murkomen.

Mashirika hayo yanataka serikali ichunguze mashambulizi yaliyotokea, ibaini waliohusika na kuhakikisha wanaowajibika wanachukuliwa hatua za kisheria.

Katika ombi lao, yanasema licha ya kuwepo kwa sheria za kukabiliana na ghasia za kisiasa, hakuna uchunguzi au mashtaka yaliyofanikiwa dhidi ya wanaopanga, kufadhili au kutekeleza mashambulizi hayo.

“Licha ya mifumo hiyo ya kisheria na kuwepo kwa ushahidi katika matukio kadhaa yaliyotajwa, hakuna uchunguzi, kukamatwa au mashtaka yaliyofanikiwa dhidi ya wahusika,” sehemu ya kesi inasema.

Jopokazi linalopendekezwa litajumuisha maafisa wa Huduma ya Kitaifa ya Polisi na Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), wakishirikiana na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma.

Litaangazia jinsi magenge yanayohusishwa na ghasia za kisiasa yanavyopangwa na kufadhiliwa, pamoja na kuwafungulia mashtaka wanaopatikana na hatia.

Mashirika hayo pia yanataka kikosi hicho kiwasilishe ripoti za mara kwa mara mahakamani kuhusu hatua zinazochukuliwa kuzuia na kuchunguza ghasia hizo.

Yanasema mazingira ya kabla ya siku ya kupiga kura ni muhimu sawa na shughuli za uchaguzi wenyewe.

Yanataja Katiba, inayotaka uchaguzi uwe huru dhidi ya ghasia, vitisho, ushawishi usiofaa na ufisadi.

“Uchaguzi unaofanyika kukiwa na ghasia nyingi na zinazoendelea kabla ya siku ya kupiga kura hauwezi kufikia kiwango cha uchaguzi usio na ghasia na vitisho,”inasema kesi ya mashirika hayo.

Mashirika hayo yametaja matukio kadhaa tangu mapema 2025, yakiwemo shambulizi katika ofisi za KHRC jijini Nairobi Julai 6, 2025, ambapo watu waliokuwa wamejihami wanadaiwa kuvuruga mkutano wa wanahabari wa mama wa waathiriwa wa ukatili wa polisi.

Pia yametaja shambulizi dhidi ya Seneta wa Vihiga Godfrey Osotsi katika mkahawa mmoja Kisumu Aprili 8, 2026, ghasia wakati wa uchaguzi mdogo wa Ol Kalou Julai 16, 2026, na shambulizi dhidi ya msafara wa Linda Mwananchi Homa Bay Agosti 16, 2026.

Baadhi ya matukio hayo yanadaiwa kuhusisha kushambuliwa kwa wanahabari na kuharibiwa au kuibwa kwa vifaa vyao.

Mashirika hayo yanasema vitisho hivyo vinaweza kuwazuia wananchi kuhudhuria mikutano, kukosoa serikali na kutumia haki zao za kukusanyika na kujieleza.

Yanaonya kuwa kutochukuliwa hatua kunaweza kudhoofisha imani ya umma katika sheria na kufanya hofu kuwa nyenzo ya ushindani wa kisiasa kuelekea uchaguzi wa 2027.