Mishale ya Serikali kwa Sifuna yaongezeka
SENETA wa Nairobi, Edwin Sifuna amekuwa mlengwa wa matamshi makali kutoka kwa viongozi wa serikali ya Kenya Kwanza, huku akizidisha juhudi za kujijenga kisiasa kuelekea kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2027.
Baada ya Rais William Ruto, Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi ndiye wa hivi punde kumkosoa Sifuna, akitilia shaka uwezo wa vuguvugu lake la Linda Mwananchi kuongoza taifa.
“Wapo wanaokuja na chama ambacho hakijamaliza hata miezi sita, wakidai ndicho kitakachotoa dira. Tusikubali aina hiyo ya pata-potea ya kisiasa,” alisema Bw Mudavadi.
Akizungumza katika kanisa la ACK, Jimbo la Kapsabet, Nandi, Jumapili, Bw Mudavadi alisema, “Wanaofikiria kuwa wanaweza kupandishwa juu kwa parachuti na kupewa uongozi nchini Kenya, ninawaambia kuwa parachuti hiyo itakatika wakiwa angani,” akaonya.
Kauli hiyo ilijiri siku chache baada ya Rais Ruto kumshambulia Bw Sifuna na washirika wake wa kisiasa.
Dkt Ruto amedai Seneta Sifuna na chama chake (The Equitable Party) kuwa hawana mwelekeo, huku akikejeli juhudi zao za kuchangisha fedha kutoka kwa wananchi.
“Mwenyewe hana kitu, chama chake hakina kitu. Halafu anaanza kuwaomba kina mama shilingi kumi kumi. Chama hicho kimekwama kwenye baa,” alisema Rais Ruto.
Ingawa Rais amekuwa akiwakosoa pia viongozi wengine wa upinzani, wakiwemo Kalonzo Musyoka, Fred Matiang’i, Rigathi Gachagua na rais mstaafu Uhuru Kenyatta, mashambulizi dhidi ya Bw Sifuna yamejitokeza kwa uwazi zaidi katika siku za hivi karibuni.
Bw Sifuna, ambaye aliwahi kuwa katibu mkuu wa chama cha ODM, sasa anajaribu kupanua ushawishi wake nje ya chama hicho huku akipigia debe Linda Mwananchi kuwa vuguvugu la kisiasa linalolenga kuleta mabadiliko katika uongozi wa nchi.
Akizungumza katika ibada ya Jumapili katika kanisa la Jesus Teaching Ministry, Donholm, Nairobi, Sifuna alijibu wakosoaji wake kwa kusema kuwa uongozi haupaswi kuamuliwa na umri, utajiri au muda ambao mtu amekuwa katika siasa. “Tutaingia katika nyumba zenu, tutaingia katika maeneo yote ya taifa hili, na kijana ambaye amechaguliwa kwa muhula mmoja pekee kama seneta ataweka historia ya kuwa rais katika taifa hili la Kenya,” alisema Bw Sifuna.
Aliongeza kuwa Wakenya hawapaswi kufungwa na dhana kuwa ni lazima mtu awe na umri fulani au kiwango fulani cha utajiri ili aweze kuwa rais.
“Watu wamezoea kuwa siasa za Kenya lazima ziendeshwe kwa njia fulani: lazima uwe na umri fulani, lazima uwe na pesa kiasi fulani,” alisema. Aliwataka wafuasi wake kueneza ujumbe wa Linda Mwananchi kote nchini, akieleza kuwa vuguvugu hilo linaweza kuongoza taifa licha ya kuwa limekuwepo kwa muda mfupi.
“Rais William Ruto, utaelewa manifesto yetu tu. Ulituambia tukupeleke pole pole, tutakupeleka pole pole lazima kitaeleweka!” alisema Bw Sifuna.
Mwanachama wa Linda Mwananchi, Brian Weke pia alimjibu Rais Ruto kwa kugeuza kejeli ya “kutokuwa na kitu” kuwa hoja kuhusu kile anachodai kuwa msimamo wa kiongozi wao dhidi ya ufisadi na dhuluma.
“Sifuna ni ‘Bw Kutokuwa na Kitu.’ Hana ufisadi, hana wizi wa mashamba, hajapiga vijana wetu risasi wala kuwanyanyasa Wakenya,” alisema Bw Weke.
Katika mjadala huo, mchambuzi wa masuala ya kisiasa, Prof Tom Namwamba anatathmini kuwa Bw Sifuna anajitokeza kuwa mshindani wa wanasiasa wa muda mrefu, hasa katika eneo la Magharibi mwa Kenya.
Kwa mujibu wa Prof Namwamba, kukosa uzoefu mkubwa wa uongozi wa kitaifa si kikwazo kinachomzuia mtu kuwa rais, kwa kuwa uamuzi wa mwisho hufanywa na wapigakura.
Alitolea mfano wa rais wa zamani wa Amerika, Barack Obama, aliyehudumu kama seneta wa jimbo la Illinois na baadaye kuchaguliwa kuwa rais mwaka wa 2008.
“Ni wananchi wanaochagua. Wakimchagua Sifuna, wakosoaji wake ni nani kupinga uamuzi huo?” alisema Prof Namwamba.
Hata hivyo, mfano huo hauondoi changamoto zinazowakabili wanasiasa wanaotaka kujenga uungwaji mkono wa kitaifa, ikiwemo kuunda kikosi, kuimarisha miundo ya chama na kuweka sera zinazoweza kuvutia wapigakura katika maeneo mbalimbali ya nchi.
Umaarufu wa Seneta wa Nairobi pia umejitokeza katika tafiti za maoni ya wananchi kuhusu uchaguzi wa urais wa 2027.
Utafiti wa Infotrak wa Julai 2026 ulimweka Rais Ruto mbele kwa asilimia 32, akifuatwa na kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka kwa asilimia 13. Seneta Sifuna na aliyekuwa Waziri wa Usalama Fred Matiang’i walishika nafasi moja kwa asilimia 12 kila mmoja.
Kwa upande mwingine, utafiti wa Trends and Insights for Africa (TIFA) uliofanywa Juni 2026 ulimpa Rais Ruto asilimia 24 ya uungwaji mkono kitaifa, huku Bw Sifuna akipata asilimia 15. Utafiti huo pia ulionyesha kuwa asilimia 44 ya wafuasi wa ODM waliohojiwa walimtaja Bw Sifuna kuwa chaguo lao la kugombea urais kwa tiketi ya chama hicho, ikilinganishwa na asilimia 20 waliomtaja Rais Ruto.
Kulingana na Prof Namwamba, matokeo hayo yanaonyesha Bw Sifuna ana uungwaji unaostahili kutiliwa mkazo katika mjadala wa kisiasa, ingawa kura za maoni pekee haziwezi kuamua matokeo ya uchaguzi.
Changamoto yake ni kugeuza uungwaji huo kuwa mtandao wa kisiasa unaovuka mipaka ya Nairobi na ngome za jadi za ODM, huku akijenga chama chenye uwezo wa kushindana katika maeneo mbalimbali ya nchi.
Kadiri uchaguzi wa 2027 unavyokaribia, mvutano kati ya Sifuna na viongozi wa Kenya Kwanza unaendeleza mjadala kuhusu nafasi ya wanasiasa wapya, uzoefu wa uongozi na uwezo wa kujenga uungwaji mkono wa kitaifa katika siasa za Kenya.