“Tuadhibuni sisi, lakini wake muwaache wake zetu,” – Waititu
ALIYEKUWA gavana wa Kiambu Ferdinand Waititu na mfanyabiashara Charles Mbuthia Chege wameomba mahakama kuwaachilia huru wake zao katika kesi ya ufujaji wa fedha zinazohusishwa na zabuni ya barabara ya Sh588 milioni.
Waititu na Chege, mkurugenzi wa kampuni ya Testimony Enterprises, walitoa ombi hilo Jumanne wakati wa kusikilizwa kwa hoja ya kupunguza adhabu katika Mahakama ya Kupambana na Ufisadi ya Milimani.
Kupitia mawakili wao, walisema Susan Wangari Ndung’u na Beth Wangechi Mburu hawakuhusika katika maamuzi ya zabuni hiyo, bali walikuwa washirika katika kampuni.
Wakili wa Waititu alisema Susan hakuwa mtiaji saini wa akaunti za kampuni wala hakushiriki katika maamuzi ya biashara. Aliongeza kuwa Beth alikuwa ametia saini tu fomu za kuanzishwa kwa kampuni na hakuwa na jukumu katika shughuli zake.
Waititu, ambaye tayari anatumikia kifungo cha miaka 12 kwa makosa yanayohusiana na ufisadi, aliomba mahakama izingatie adhabu ambayo tayari wamepitia.
Alisema adhabu inapaswa kurekebisha mkosaji badala ya kuharibu maisha yake, akitaka mahakama iwape nafasi nyingine.
Chege naye alisema mkewe alikuwa na hisa moja pekee katika kampuni na hakuwa na mamlaka ya kutia saini akaunti za benki. Alisema alikuwa akitumikia adhabu ya kifungo cha miaka 11 au kulipa faini ya Sh296 milioni.
Hata hivyo, upande wa mashtaka ulipinga ombi hilo, ukisema kila mshtakiwa anapaswa kuwajibika kwa makosa aliyopatikana nayo na kuadhibiwa kwa mujibu wa sheria.
Jaji wa Mahakama Kuu Rose Ougo alibadilisha uamuzi wa kuwaachilia huru washtakiwa kwa makosa ya ulanguzi wa fedha, akisema mahakama ya awali ilikosea kutathmini ushahidi na sheria.
Waititu alipatikana na hatia ya kupokea Sh25 milioni kwa njia ya ufisadi kutoka kwa kampuni iliyopata zabuni ya barabara ya thamani ya Sh588 milioni.
Mahakama inatarajiwa kutoa adhabu kwa washtakiwa hao wanne Novemba 2.