HabariHabari za KauntiHabari za Kitaifa

Wataka Mackenzie wa Shakahola anyongwe!

Na BRIAN OCHARO November 4th, 2026 Kusoma ni dakika: 3

MHUBIRI aliyepatikana na hatia ya mauaji Shakahola, Paul Nthenge Mackenzie, ameiomba Mahakama imhurumie anaposubiri kuhukumiwa Ijumaa.
Hayo yamejiri huku upande wa mashtaka ukitaka apewe hukumu ya kifo, na washtakiwa wenzake wafungwe maisha gerezani.
Mahakama Kuu ilimpata na hatia ya mauaji ya watoto 190 na mtu mzima mmoja katika Msitu wa Shakahola, kati ya Januari 2021 na Septemba 2023.
Mackenzie sasa amemweleza Jaji Diana Kavedza kuwa yeye na washitakiwa wenzake 28 pia ni waathiriwa wa mkasa huo, ambapo jumla ya watu 429 walifariki dunia wakiamini kuwa walikuwa wakijiandaa kwenda kumwona Yesu.
“Kwa namna fulani, tulipoteza mali na watoto wetu. Jambo ambalo tunalijutia, na tunaomba mahakama hii ituhurumie na kulizingatia kabla ya kutupatia adhabu kali,” alisema kupitia kwa wakili wake.
Washtakiwa hao waliiomba mahakama izingatie hali zao binafsi na mabadiliko ambayo wanasema wamepitia wakiwa kizuizini. Walieleza kuwa vifo hivyo vilikuwa janga kubwa lisilopimika na kusisitiza kuwa hawakuwa na nia ya kupuuza maumivu ya familia zilizowapoteza wapendwa wao.
Washtakiwa hao walisema majuto yao yanapaswa kupimwa kwa kuzingatia mwenendo wao, kutambua makosa yaliyotendeka na utayari wao wa kubadilika. Walisisitiza kuwa adhabu inapaswa kuzingatia uzito wa makosa pamoja na wajibu wa kila mshukiwa na nafasi yake ya kurekebisha mwenendo wake.
“Adhabu inayotoa nafasi ya mtu kujirekebisha si ishara ya udhaifu,” walisema.
Washitakiwa walisema wamekuwa kizuizini tangu 2023, ambapo wameshiriki katika mipango ya kidini na mafunzo mengine. Waliiomba mahakama izingatie pia ushiriki wao katika mipango ya kuwaondoa watu katika misimamo mikali ya kidini iliyofanyika kati ya Agosti 20 na 23, 2025, wakisema hatua hiyo inaonyesha utayari wao wa kubadilika na kurejea katika jamii.
Pia, walieleza kuwa mitazamo yao ya kidini imebadilika tangu walipokamatwa, na kuiomba mahakama izingatie mabadiliko hayo pamoja na ripoti za tathmini kabla ya hukumu kutolewa.
Waliomba mahakama izingatie huruma, haki na uwiano wa adhabu, huku ikitoa nafasi kwa haki inayolenga kurekebisha madhara yaliyotokea.
“Tunapendekeza kifungo kisichozidi miaka 10, huku muda ambao washtakiwa wamekwishatumia kizuizini ukizingatiwa,” alisema wakili wao.
Hata hivyo, upande wa mashtaka uliomba washtakiwa wote wahukumiwe vifungo vya gerezani na washirikishwe katika mpango maalumu wa kurekebisha mwenendo wao, ukisema hawajaonyesha majuto.
Kulingana na upande wa mashtaka, washtakiwa wote isipokuwa Enos Amanya Ngala wameendelea kukana mashtaka. Bw Ngala alikiri kushiriki katika mauaji hayo.
“Wameendelea kukana mashtaka, kukataa kuwajibika kwa uhalifu huo na kuyatafsiri mashtaka dhidi yao kwa namna hasi. Kwa hakika, washtakiwa hawakuonyesha majuto wala kujutia matendo yao. Pia inashangaza kwamba bado wanashikilia mafundisho yaliyochangia vifo hivyo,” upande wa mashtaka ulisema.
Serikali ilipendekeza adhabu zitakazoakisi uzito na ukubwa wa makosa hayo. Kwa Bw Ngala, ilipendekeza kifungo cha miaka 11, muda aliokuwa ametumikia kizuizini tangu Aprili 2023 ukizingatiwa.
Pia ilipendekeza afanyiwe mpango wa marekebisho ya tabia akiwa gerezani kwa kipindi cha kati ya miezi 24 na 30, huku ripoti za anavyoendelea zikiwasilishwa mara kwa mara ili kusaidia tathmini ya baadaye ya adhabu yake.
Kwa Mackenzie, upande wa mashtaka uliomba mahakama itoe adhabu ya kifo, huku washtakiwa wengine 27 wakihukumiwa kifungo cha maisha gerezani.
“Upande wa mashtaka unaunga mkono kutolewa kwa adhabu ya kifo kwa Mackenzie, kwa kuzingatia pia maelezo yake ya kujitetea , majuto yake na uwezekano wa kurekebisha mwenendo wake,” alisema  Mkurugenzi Msaidizi wa Mashtaka ya Umma, Bw Jami Yamina.
Upande wa mashtaka ulisema adhabu inapaswa kuzingatia malengo ya haki ya jinai, yakiwemo kuadhibu, kuzuia uhalifu wa aina hiyo, kulinda umma, kukemea uhalifu, kurekebisha madhara na kuwasaidia wahusika kubadilika.
Pia ulipendekeza waathiriwa wagawanywe katika makundi matatu ya umri: watoto wenye umri wa hadi miaka saba, wale wa miaka minane hadi 14, na walio na umri wa miaka 15 hadi 18.
Aidha, uliwasilisha pendekezo la Kituo cha Kitaifa cha Kukabiliana na Ugaidi (NCTC), kilichopendekeza washitakiwa washiriki kwa hiari katika programu za marekebisho ya misimamo mikali na kupewa mafundisho mbadala ili kuwawezesha kurejea katika jamii.
Mwezi uliopita, Mahakama Kuu ilimpata Makenzie na wenzake 28 na hatia ya kuwaua watoto 190 na mtu mzima mmoja katika msitu wa Shakahola. Watu hao watapewa kifungo chao Novemba  6.