Jamvi La Siasa

Upinzani unavyojitoa pumzi kwa kulumbana hadharani

Na Benson Matheka November 8th, 2026 Kusoma ni dakika: 3

Viongozi wa upinzani wanaotaka kumwondoa Rais William Ruto mamlakani katika uchaguzi wa 2027 wanaonekana kutumia nguvu nyingi kujibizana hadharani, huku tofauti kuhusu nani atakayepeperusha bendera ya muungano na namna ya kugawana mamlaka zikizidi kujitokeza.

Wachanganuzi wa siasa wanasema badala ya kuonyesha umoja na kuelekeza nguvu zao katika kuandaa ajenda mbadala ya taifa, baadhi ya vinara hao sasa wanashambuliana kwa maneno, wakilaumiana kwa kuwa na kiburi, ubabe na kujaribu kumiliki uongozi wa upinzani.

“Badala ya kuonyesha ushirikiano wao unapata nguvu kuelekea muungano, wanarushiana cheche za maneno hadharani. Wanabomoa Imani ya wafuasi wao kwao,” asema mchanganuzi wa siasa Daniel Kioko.

Kulingana na kiongozi wa Jubilee Jeremiah Kioni, migawanyiko hiyo inaweza kumpa Rais Ruto nafasi ya kunufaika na kura kati ya wagombeaji wengi wa urais.

Akizungumza katika mahojiano na kituo cha redio Alhamisi, Novemba 5, Kioni alisema viongozi wanaowania urais katika vyama tofauti wanahatarisha azma ya kuwa na mgombeaji mmoja wa kumkabili Rais Ruto.

“Ni njia gani bora ya kumpa muhula wa pili? Hiyo ndiyo njia bora kabisa. Kwa kweli, atafurahi,” alisema Kioni, akirejelea uwezekano wa vinara wa upinzani kuingia katika uchaguzi ujao wakiwa kadhaa.

Alitaja aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’i, aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka na Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna miongoni mwa wanasiasa ambao misimamo na matarajio yao yanaweza kuathiri mazungumzo ya kuunda muungano.

Mvutano huo ulijitokeza wazi baada ya Gachagua kupendekeza muungano unaowaleta pamoja yeye, Sifuna na Kalonzo, akisema viongozi hao wana idadi ya kutosha ya wapiga kura kumkabili Rais Ruto.

Katika mahojiano na runinga ya Inooro, Gachagua alidai kuwa anaweza kuleta kura milioni 10, Sifuna milioni nne na Kalonzo milioni tatu. Alilinganisha mpango huo na ushirikiano wa kisiasa kati ya marehemu Mwai Kibaki na Kijana Wamalwa uliosaidia upinzani kushinda uchaguzi wa 2002.

Hata hivyo, pendekezo hilo lilionekana kuwaacha nje baadhi ya vinara wengine, akiwemo Matiang’i, Martha Karua, Eugene Wamalwa na Justin Muturi.

Matiang’i alijibu kwa kulaumu Gachagua kwa kutumia kiburi na majivuno yanayoweza kuvunja upinzani. Alipinga pia siasa zinazotegemea hesabu za kikabila badala ya sera, uwezo na rekodi za viongozi.

“Uongozi na mustakabali wa nchi yetu haupaswi kuamuliwa kwa kugawanya watu kwa misingi ya makabila. Nilidhani huu ni ushindani wa mawazo, sera za maendeleo, rekodi, uwezo na sifa,” alisema Matiang’i.

Aliongeza kuwa yuko tayari kumuunga mkono mgombeaji yeyote atakayechaguliwa kupitia mchakato shirikishi na unaokubalika, lakini akapinga viongozi wachache kuwalazimisha wengine kukubaliana na chaguo lao.

“Hakuna Mkenya anayepaswa kuachwa nyuma. Lazima tuwashirikishe wote,” alisema katika mahojiano na NTV.

Gachagua, hata hivyo, alijitetea dhidi ya madai ya kiburi, akisema kuwa baadhi ya wanasiasa humchukulia kuwa mkorofi kwa sababu anasema ukweli. Alisisitiza kuwa kampeni za urais zinahitaji kuzingatia idadi ya kura na uwezo wa kuunganisha maeneo yenye wapiga kura wengi.

Mzozo huo pia umehusisha Muturi, ambaye alimtaka Gachagua kuelewa kuwa hakuna jamii moja inayoweza kumuingiza mtu Ikulu bila ushirikiano kitaifa.

Kwa mujibu wa Muturi, muungano wa upinzani unapaswa kujengwa kwa kuheshimiana badala ya vitisho, ubabe na mashindano ya kuonyesha nani ana nguvu zaidi.

Changamoto nyingine ni kukubaliana kuhusu mgombeaji wa urais. Hadi sasa, mazungumzo ya viongozi hao hayajazaa makubaliano ya mwisho kuhusu atakayebeba bendera ya upinzani, huku baadhi wakitaka uamuzi ufanywe mapema ili maandalizi ya kampeni yaanze.

Kwa sasa, Kioni na Matiang’i wanaonya kuwa muda unaotumika katika malumbano unaweza kuathiri juhudi za kujenga timu moja. Hata hivyo, wachanganuzi wa siasa wanasema kwamba suala linalowakabili viongozi hao si kuchagua mgombeaji pekee, bali pia kukubaliana kuhusu sera, uwakilishi wa maeneo mbalimbali na namna ya kushirikiana bila mmoja kuhisi ametengwa.

“Huku uchaguzi wa 2027 ukikaribia, swali kubwa ni iwapo vinara hao wataweza kuweka kando tofauti zao na kufikia makubaliano, au wataendelea kulumbana huku kila mmoja akijaribu kuthibitisha ubabe wake wa kisiasa,” asema mchanganuzi wa siasa Deborah Muyaki.