Kalonzo aingia baridi baada ya Gachagua kumkaribisha Ngilu nyumbani Wamunyoro
USHIRIKIANO unaochipuka kati ya kiongozi wa DCP Rigathi Gachagua na Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna huenda ukazua ushindani mpya wa kisiasa katika ngome ya kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, baada ya aliyekuwa Gavana wa Kitui Charity Ngilu kuingia kwenye hesabu za upinzani kuelekea uchaguzi wa 2027.
Mkutano wa Gachagua na Ngilu nyumbani kwake Wamunyoro Jumanne umeibua maswali kuhusu mikakati ya kuunganisha Mlima Kenya, Magharibi na maeneo ya Kusini Mashariki ili kuunda muungano wenye nguvu za kumkabili Rais William Ruto.
Gachagua alilinganisha mazungumzo hayo na muungano wa National Rainbow Coalition (NARC) uliofanikisha kuondoa KANU madarakani mwaka 2002 baada ya kutawala kwa miaka 40.
Alikumbuka jinsi aliyekuwa rais marehemu Mwai Kibaki alivyoshirikiana na marehemu Michael Kijana Wamalwa wa Magharibi, huku Ngilu akiwa miongoni mwa viongozi walioungana kumng’oa KANU.
Washirika wa Gachagua na Sifuna wanasema wanataka kufufua mkakati huo kupitia kile wanachokiita “Muungano wa Milima”, unaolenga kuunganisha Mlima Kenya na eneo la Mlima Elgon, ambako Sifuna ana ngome yake ya kisiasa.
Aidha, wanataka kupanua ushawishi wao katika Kusini Mashariki, eneo ambalo Kalonzo amekuwa na ushawishi mkubwa kupitia chama cha Wiper.
Mmoja wa maafisa wa kambi hiyo aliambia Taifa Leo kuwa wanatambua uwezo wa kura za Mlima Kenya na Magharibi na wanataka maeneo hayo yawe nguzo za muungano wao.
Alidokeza kuwa Ngilu anaweza kusaidia kuvutia wafuasi wa Kusini Mashariki iwapo Kalonzo hatakubaliana na mpango wao.
Hata hivyo, hatua ya Ngilu kukutana na Gachagua imezua hasira katika kambi ya Kalonzo.
Seneta wa Kitui Enoch Wambua alimshutumu Ngilu kwa kutaka kudhoofisha azma ya Kalonzo kuwania urais.
Alimtaja kama mwanasiasa anayebadilisha misimamo kwa manufaa binafsi na kudai mkutano wa Wamunyoro ulilenga kuunda kituo kingine cha nguvu za kisiasa kushindana na Wiper eneo hilo.
Wambua pia alidai Ngilu aliwahi kushirikiana na wapinzani wa Kalonzo katika uchaguzi uliopita ili kushinikiza uwezo wake wa kuwa naibu wa marehemu Raila Odinga upimwe kupitia kinachofahamika kama mahojiano.
Lakini Seneta wa Makueni Dan Maanzo alimtetea Ngilu, akisema bado ni sehemu ya mashauriano ya upinzani na hakuna njama iliyofichwa katika mkutano huo.
Maanzo alionya kuwa hakuna jamii moja au mbili zinazoweza kushinda uchaguzi wa urais pekee, akisema upinzani haupaswi kupoteza chama, mgombeaji au hata kura moja.
Naibu Kiongozi wa DCP Cleophas Malala amekuwa akitetea muungano wa Mlima Kenya na jamii ya Mulembe, akisema lengo ni kuunganisha wapinzani ili kumbwaga Ruto.
Hata hivyo, Gachagua amejitenga na matamshi ya Malala, akisema hayawakilishi msimamo rasmi wa chama.
Mvutano mwingine unahusu nani anafaa kuongoza upinzani katika uchaguzi wa 2027.
Wakati wa uzinduzi wa makao makuu ya Linda Mwananchi, Kalonzo alionya dhidi ya kutangaza mgombeaji mapema kabla ya mashauriano na taratibu rasmi za vyama kukamilika.
Alisema Sifuna anafaa kusubiri uamuzi wa Kongamano la Kitaifa la Wajumbe wa Linda Mwananchi Movement (LMM) lililopangwa Novemba 13.
Kwa upande wake, viongozi wa Wiper katika Pwani wamesisitiza kuwa Kalonzo anapaswa kuwania urais mwenyewe iwapo hatapewa tiketi ya pamoja ya upinzani, wakipinga uwezekano wa kuwa mgombeaji mwenza wa kiongozi mwingine.
Mkutano wa Ngilu na Gachagua kwa hivyo umeongeza mwelekeo mpya katika mazungumzo ya upinzani.
Hata hivyo, bado hakuna makubaliano rasmi kuhusu mgombeaji mmoja, ugavi wa nafasi za uongozi au muundo wa muungano.
Wachambuzi wanasema changamoto kubwa kwa wapinzani ni kugeuza mikutano na kauli za kisiasa kuwa makubaliano yatakayoruhusu viongozi wenye matarajio tofauti kufanya kazi pamoja bila kudhoofisha ngome zao.