Habari

Mitetemeko ya ardhi yazua hofu nchini

March 24th, 2019 1 min read

Na WANDERI KAMAU

MITETEMEKO kadha y ardhi ilishuhudiwa katika sehemu mbalimbali nchini Jumapili jioni, hali iliyozua hofu na wasiwasi miongoni mwa Wakenya waliokuwa wakiendelea na shughuli zao za kawaida.

Hali hiyo ilianza baada ya umeme kuripotiwa kupotea katika mji wa Kitui, ila ikafuata katika sehemu zingine nchini.

Jijini Nairobi, watu mbalimbali walisema walihisi majengo walimokuwa yakitisika katika hali isiyokuwa ya kawaida.

“Nilikuwa kazini katika Jumba la Nation. Ghafla, nilisikia jengo hilo likitikisika, hali ambayo si ya kawaida. Mtikiso huo ulidumu kwa sekunde chache,” akasema Bernadine Mutanu, mwandishi wa shirika la habari la Nation Media Group.

Mitetemeko hiyo pia iliripotiwa katika maeneo ya Nairobi, Wundanyi, Mombasa, Makueni, Embu, Nyeri, Meru kati ya sehemu zingine.

Kwenye taarifa, Idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa, Nairobi ilithibitisha mitetemeko hiyo, ila ikasema kwamba hakuna uharibifu wowote uliosababishwa nayo.

Hata hivyo, kulizuka mijadala ya ikiwa huenda hali hiyo ikawa “timio” la “utabiri” wa ‘Nabii’ David Owuor, aliyesema Jumapili kwamba anaona Kenya na sehemu zingine duniani zikikumbwa na hali ya misukosuko.

“Ninaona Kenya na sehemu zingine zikikumbwa na nyakati ngumu. Ni lazima Wakenya watubu kutokana na dhambi kama ufisadi, ukabila, kutusiana kati ya zingine ili Mungu aweze kuiokoa nchi,” akasema Dkt Owuor.

Vile vile kulikuwa na mijadala ya ikiwa huenda hali hiyo ni matukio ya kawaida ya maumbile ya dunia.

Nchi zingine zilizoshuhudia tetemeko hilo ni Colombia, Indonesia, Turkey na Uhispania.