Habari

Weupe wa Weke wasababisha farakano hafla ya harambee

May 31st, 2019 1 min read

Na CHARLES WASONGA

KIOJA kilishuhudiwa katika mkutano mmoja wa harambee katika Shule ya Upili ya Father Tilen katika eneobunge la Suba Kaskazini baada ya mwanasiasa mmoja kudai kuwa mwanasiasa Brian Weke ni wa asili ya China.

Jim Akali ambaye aliwania kiti hicho cha ubunge katika uchaguzi mkuu uliopita na akaangushwa na Bi Millie Odhiambo Mabona, alidai kuwa alipozuru China mwaka 2018 alipita karibu na “nyumbani kwa akina Weke.”

“Nataka kumwambia Weke mchana peupe nilipozuru China majuzi nilipitia kando ya boma la wazazi wake katika mji mmoja ambao hata nashindwa kutamka jina lake,” akasema Bw Akali akiongeza kuwa weupe wa Bw Weke ni ishara kuwa yeye “sio Msuba bali ni Mchina.”

Mwanasiasa huyo aliongeza kuwa Bi Mabona hafai kumpa Weke nafasi ya kuendesha masuala ya eneobunge hilo kwani hatoki jamii yao ya Abasuba.

Akijibu Bw Weke alikana dai kwamba yeye ni Mchina akiongeza kuwa wazazi wake wote ni Wasuba.

Alisema weupe wake ni kiashiro cha utanashati wala sio eti yeye ni Mchina.

“Weupe wangu ni ishara ya utanashati. Haufai kutumiwa na yeyote kunitenga na watu wangu wa Suba Kaskazini,” akasema.

Ni makosa

Huku akionekana mwenye hasira, Bw Weke alisema ni makosa kwa mtu yeyote kudai yeye ni Mchina akisema kwao ni Suba Kaskazini.

Kumekuwa na madai kuwa Bi Mabona ana uhusiano wa kimahaba na Weke lakini mwanasiasa huyo ambaye pia ni mwanaharakati wa kutetea haki za kibinadamu alipuuzilia mbali madai hayo akisema mbunge huyo ni shangazi yake.

“Millie amekuwa kama mshauri wangu. Nataka kusema wazi kwamba Mheshimiwa Millie ni shangazi yangu. Babu yangu na babake ni kaka,” akasema.