Habari

DCI yaagizwa ichunguze kifo cha wakili Karanja Kabage

July 6th, 2019 1 min read

Na JOEL MUINDE

INSPEKTA Mkuu wa Polisi Hillary Mutyambai ameagiza uchunguzi wa kifo cha wakili na mfanyabiashara Karanja Kabage ambaye alihusika katika ajali Ijumaa usiku jijini Nairobi.

“Tunashauri pawepo utulivu wakati tunajitahidi kubainisha kiini hasa cha kifo chake,” inasema sehemu ya taarifa kutoka idara ya polisi iliyotolewa Jumamosi.

Pia ripoti hiyo imefichua kwamba Kabage alikuwa mwenyewe katika gari akiliendesha katika Southern Bypass pale “gari lake lilienda katika sehemu isiyofaa ya barabara, likapunguza kasi na kisha kuonekana likipinda kuelekea sehemu lilikuwa linatoka kabla ya kugonga nguzo.”

Baada ya tukio hilo, polisi wanasema Kabage aliomba watu wawili waliosimama kumsaidia, akiwataka wampeleke hospitalini.

“Dereva wa teksi alisimamisha gari lake na kujiunga nao. Mwathiriwa aliomba apelekwe katika Nairobi Hospital. Dereva wa teksi alichukua udhibiti wa Land Cruiser na kumpeleka mwathiriwa katika Nairobi Hospital. Waliandamana na mtu mwingine aliyejitolea kusaidia ambaye aliendesha gari la pili,” imesema ripoti ya polisi.

Hata hivyo mara alipofikishwa hospitalini, polisi wanasema Kabage alikuwa amepoteza fahamu na juhudi za madaktari hazikuweza kumsaidia kurejelea hali nzuri.