Michezo

FKF yaitaka serikali kujenga viwanja vya kisasa kuiwezesha kuandaa mashindano

August 28th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na Geoffrey Anene

SHIRIKISHO la Soka la Kenya (FKF) limeapa kutotuma maombi ya kuandaa mashindano yoyote ya kimataifa hadi pale serikali itakuwa na viwanja vya kisasa.

Akizungumza jijini Nairobi hapo Agosti 28 baada ya Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF) kukataa ombi la Kenya kuwa mwenyeji wa Kombe la Afrika la Wanawake (AWCON) mwaka 2018, Rais wa FKF Nick Mwendwa hajaficha masikitiko yake Kenya kunyimwa mashindano tena kutokana na ukosefu wa viwanja.

“Hatutaomba tena uenyeji wa mashindano yoyote ya kimataifa hadi pale viwanja vitakuwa tayari. Serikali ilituunga mkono kuomba CAF ilete Kombe la Afrika la wanawake nchini Kenya, lakini baada ya wakaguzi kutoka CAF kuzuru viwanja vyetu, ni uwanja wa Kasarani pekee ndio umeidhinishwa kuandaa mashindano ya kimataifa.

Tulihitaji viwanja viwili vya kisasa. Tulitumai uwanja wa Kenyatta mjini Machakos utakubaliwa, lakini Kasarani pekee ndio ulipita mtihani wa wakaguzi hao. Mashindano ya kimataifa ya wanaume yanahitaji viwanja vinne kwa hivyo hatuwezi kuomba kuandaa mashindano yoyote makubwa.

Tulitamani sana kuomba mashindano ya dunia ya chipukizi, lakini hatuwezi kufanya hivyo kwa sababu hatuna viwanja. Tunajaribu kusukuma Serikali kuhakikisha viwanja viko sawa.

Tunatumai uwanja wa kitaifa wa Nyayo utakuwa umefanyiwa ukarabati kufikia mwisho wa mwaka huu na hata ule wa Kinoru na viwanja vingine. Kwa sasa, hatutaomba mashindano yoyote hadi viwanja viwe tayari,” Mwendwa amesema.

FKF, ambayo ilifahamu miezi kadhaa iliyopita kwamba Ghana itapokonywa uenyeji wa Kombe la Afrika la Wanawake, iliandikia CAF barua ya maombi.

CAF kisha ilituma wakaguzi kuangalia viwanja vya Kenya. Tulipokea ripoti juma lililopita kwamba hatuwezi kuwa wenyeji kwa sababu tuna uwanja mmoja pekee – Kasarani. Uwanja wa Kenyatta haukutimiza viwango vinavyohitajika vya vyumba vya kubadilishia nguo pamoja na mipango kabambe ya usalama.

Mwendwa ameambia wanahabari Jumanne kwamba alikutana na Rais wa CAF Ahmad Ahmad wikendi iliyopita na kufahamishwa tena Kenya haina viwanja vya kutosha vinavyoweza kuandaa mashindano makubwa.

Kenya iliwahi kuomba uenyeji wa mashindano ya soka ya wachezaji wanaosakata katika mataifa yao almaarufu CHAN mwaka 2018.

Ombi lake lilifaulu Februari mwaka 2016, lakini baada ya CAF kuzuru Kenya mara kadhaa, Kenya ilipokonywa haki za kuandaa mashindano hayo kutokana na ukosefu wa viwanja, miongoni mwa sababu zingine.

Mbali na kuamua kutoomba mashindano yoyote makubwa kuletwa Kenya, Mwendwa amesema FKF imeandikia Shirikisho la Soka la Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) ikitaka isifanywe kuwa mwenyeji wa shindano lolote la eneo hili hadi viwanja viwe sawa.