BEI YA MAFUTA: Wakenya wachemka
Na BENSON MATHEKA
Hatua ya Serikali kukaidi bunge na kutoza Wakenya ushuru zaidi wa mafuta, imeshutumiwa vikali huku baadhi ya Wabunge wakitisha kuandamana iwapo hautaondolewa.
Ushuru huo tayari umesababisha nauli kupanda na inatarajiwa bei za bidhaa kupanda kwa asilimia kubwa.
Wabunge wa upande wa serikali na upinzani, waliteta kwamba, ushuru huo utasababisha mfumko wa gharama ya maisha nchini na kuwa mzigo kwa Wakenya wa kawaida.
Jana, baadhi ya Wabunge wa chama cha ODM, walimpatia Waziri wa Fedha, Bw Henry Rotich, saa 72 kusimamisha utekelezaji wa ushuru huo au waongoze Wakenya kuandamana na kumtimua.
Mnamo Ijumaa, Bw Rotich alisema ni lazima ushuru huo utekelezwe licha ya Wabunge kupitisha mabadiliko katika sheria ya fedha ya mwaka huu.
Wakiongea katika kanisa la Daniel Comboni, mtaani Mathare, Nairobi, wabunge Antony Oluoch (Mathare), Caleb Amisi (Saboti) na Mark Nyamitta (Uriri) walimshtumu Bw Rotich kwa kupuuza uamuzi wa bunge.
“Unapotoza mafuta ushuru, unaumiza moja kwa moja watu wengi masikini,” alisema Bw Nyamitta.
Mnamo Ijumaa, Tume ya Kudhibiti Nishati (ERC) iliongeza bei za mafuta kwa kutoza ushuru mpya alivyoagiza Bw Rotich. Wakenya walimwaga hasira zao mtandaoni huku baadhi ya wabunge wakimtaka Spika wa bunge kuitisha kikao spesheli kumjadili Bw Rotich.
Mbunge wa Belgut, Nelson Koech, alimwandikia barua Spika Justin Muturi, kupitia kiongozi wa wengi Aden Duale, akimtaka kuitisha kikao hicho mara moja ili kujadili na kusuta watu ambao alisema, wamekosa kuelewa athari za bei mpya za mafuta kwa uchumi wa nchi.
Kabla ya kwenda mapumzikoni Alhamisi, wabunge waliondoa vipengele katika mswada wa fedha ambavyo vingefanya Wakenya kubeba mzigo zaidi kwa kutozwa ushuru wa mafuta wa asilimia 16.
Seneta wa Makueni Mutula Kilonzo, aliuliza iwapo Bw Muturi ataitisha kikao cha bunge kujadili waziri Rotich kwa kupuuza uamuzi wa wabunge.
Mwenzake wa Baringo Gedion Moi, alisema hata ingawa serikali inahitaji pesa, athari za ushuru huo ni mbaya kwa uchumi. “Ingawa serikali inahitaji pesa kufadhili miradi yake, ushuru huo utafanya gharama ya maisha kupanda, watu kupoteza ajira na uchumi kudorora,” alisema Bw Moi kwenye taarifa.
Lakini akiongea eneo la North Horr Marsabit jana, Naibu Rais William Ruto alisema serikali itashirikiana na bunge kuhakikisha ushuru huo hautaumiza Wakenya.
Wadau katika sekta ya matatu na wanaharakati, pia waliendelea kumshutumu Bw Rotich na kutaka afutwe kazi. Chama cha watumiaji bidhaa nchini, COFEK, kilisema itakuwa vigumu kwa serikali kutimiza malengo yake ikiendelea kuwaumiza Wakenya.
“Tusemezane ukweli jameni, unawezaje kuafikia Ajenda Nne Kuu ikiwa serikali inasababishia Wakenya uchungu kama huu,” Cofek iliuliza kwenye Twitter.