Makala

TAHARIRI: Maeneobunge ya sasa yapunguzwe

September 4th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

NA MHARIRI

TUME Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) inapojitayarisha kufanya ukaguzi wa mipaka mwaka 2019, mojawapo ya mapendekezo ambayo yamejitokeza ni kupunguza idadi ya maeneobunge.

Kumeibuka mjadala kuhusu iwapo ni sawa kupunguza maeneo ya uwakilishi bungeni au wananchi waongezewe wabunge, ili kuwa na uwakilishi zaidi. Mjadala huu umezuka mwaka mmoja kabla ya shughuli yenyewe huku wanasiasa wakilumbana kuhusu jambo hilo.

Kulingana na mapendekezo yaliyopo, maeneo bunge yasiyofikisha kiwango fulani cha idadi ya wapiga kura, yanafaa kuunganishwa na mengine au kuondolewa kabisa.

Baadhi ya maeneo ambako tayari wanasiasa wameingiwa na wasiwasi ni Lamu Mashariki na Lamu Maghaibi, ambayo hata yakiunganishwa pamoja, hayafikishi wapiga kura 20,000.

Wanasiasa wa kaunti hiyo wameanza kupiga kelele, wakidai kuwa kupunguzwa mwa maeneo bunge hayo mawili kutawanyima wakazi nafasi ya kuwakilishwa vyema. Kelele sawa na hizo zinatarajiwa katika maeneo bunge mengine yenye idadi ndogo ya watu.

Madai ya wanasiasa hao hayana msingi. Kinyume na zamani ambapo maeneo bunge yalitumiwa kuwapa wananchi maendeleo kupitia hazina ya CDF, sasa hivi maendeleo yote mashinani yanafanywa kupitia serikali za kaunti.

Ni wabunge wa kaunti (MCAs) na gavana wanaoketi chini na kuwajumuisha wananchi kwenye mikutano ya kuamua miradi inayostahili kupewa kipaumbele.

Kwa sababu hiyo, haijalishi kama kaunti ina maeneo bunge kumi au eneo bunge moja, kwa sababu kilicho muhimu ni raslimali inayosambazwa na Tume ya Ugavi wa Raslimali kwa kila kaunti.

Wajibu wa wabunge kwa sasa ni kuketi bungeni na kubuni sheria. Jambo hili halihitaji wawakilishi wa maeneo bunge 290, wabunge wanawake 47 na wengine kadhaa wa kuteuliwa na vyama vya kisiasa.

Wananchi wanapaswa kujua kuwa maendeleo hayaji katika maeneo yao kupitia wabunge. Isitoshe, pesa zitakazookolewa kutokana na mishahara na marupurupu ya wabunge wengi, zitatumwa katika kaunti kuendeleza miradi muhimu.

Wakati umefika kwa wananchi kutafakari mzigo wa ushuru wanaotozwa, ambao sehemu kubwa huishia kuwa mishahara na maisha mazuri ya wabunge, ambao baadhi hawajaunda hata sheria moja ya kuwafaa watu wanaowawakilisha.