Hatimaye kesi ya Harambee Starlets dhidi ya Equatorial Guinea kuamuliwa
Na Geoffrey Anene
HARAMBEE Starlets itafahamu Septemba 8, 2018 hatima yake ya kushiriki Kombe la Afrika la Wanawake (AWCON) mwaka 2018.
Taarifa kutoka makao makuu ya Shirikisho la Soka la Bara Afrika (CAF) jijini Cairo nchini Misri zinasema kwamba malalamishi ya Kenya kuhusu mchezaji wa Equatorial Guinea Celestina Manga Besecu yalikubaliwa baada ya FKF kulipa ada ya malalamishi ya Sh200,000. Yatasikizwa na Bodi ya Nidhamu hapo Jumamosi.
FKF inaamini majina kamili ya Bescu ni Fadimatou Veronique Nsongone na wala si Celestina Manga Besecu. Inaamini Celestina Manga Besecu na Fadimatou Veronique Nsongone ni mchezaji mmoja. Equatorial Guinea ilitumia Besecu katika mechi zake. Kenya inaamini yeye ni Mkamerun.
Starlets ilishiriki AWCON kwa mara yake ya kwanza kabisa mwaka 2016 nchini Cameroon. Kampeni yake ya kushiriki AWCON kwa mara ya pili mfululizo iligonga mwamba ilipobanduliwa nje na Equatorial Guinea kwa jumla ya mabao 3-2 katika raundi ya pili.
Equatorial Guinea ilifuzu kushindania taji pamoja na Afrika Kusini, Zambia, Cameroon, Mali, Algeria na mabingwa watetezi Nigeria. Ghana pia ilifuzu, lakini kama wenyeji. Ilitupwa nje baada ya kupokonywa uenyeji.
Majuma machache yaliyopita, Kenya ilipokoea ripoti kutoka kwa CAF kwamba haiwezi kuandaa AWCON mwaka 2018 kutokana na ukosefu wa viwanja vya kisasa.
Uwanja wa kimataifa wa Kasarani pekee ndiyo unatimiza viwango vinavyohitaji kwa mashindano makubwa. Kenya ilikuwa imeomba kupewa majukumu ya kuandaa fainali hizo za AWCON mwezi Novemba/Desemba mwaka huu wa 2018. CAF bado haitangaza mwenyeji mpya.