Hatujaonja hata peni kutokana na mauzo ya Walusimbi – Rachier
HATUJAPOKEA senti yoyote kutoka kwa mibabe wa soka ya Afrika Kusini, Kaizer Chiefs baada ya uhamisho wa difenda Godfrey Walusimbi, ndiyo kauli ya Mwenyekiti wa Gor Mahia Ambrose Rachier kwenye kikao na wanahabari Jumatatu Septemba 24 jijini Nairobi.
Mlinzi huyo wa kushoto alihama Gor kwa kima cha Sh12 milioni mwezi Agosti 2018, fedha ambazo sasa uongozi wa K’Ogalo unasema hazijawafikia wala hawajabainisha ni lini zitalipwa.
Kumekuwa na ripoti zinazokinzana kuhusu hela hizo huku baadhi ya maafisa wa klabu wakidai zimefujwa na uongozi wa klabu.
Kuhusu malimbikizi ya mshahara wa mwezi Agosti ambayo yamesababisha mgomo kambini mwa masogora hao, Rachier alirejesha tabasamu nyusoni mwa kambi ya K’Ogalo alipodai fedha hizo zitalipwa kwa akaunti ya kila mchezaji leo.
“Tunaenda kulipa mishahara yao leo,” akasisitiza Rachier wakati wa mkao huo.
“Wachezaji wamepokea mshahara hadi Julai 31. Naamini wamekuwa wakichochewa ili wasihudhurie vipindi vya mazoezi kwasababu kucheleweshwa kwa mishahara si jambo geni hapa Kenya,” akaongeza Rachier.
Wachezaji wa K’Ogalo hawajakuwa wakishiriki mazoezi kwa muda wa wiki mbili kutokana na njaa iliyowasakama hadi kufikia kiasi cha kutoweza kulipa nauli ya kuwafikisha mazoezini na kuwajibikia mechi za KPL huku taarifa zikienea kwamba wengine wao walifungiwa nyumba na malandlodi kwa kutolipa kodi.