Tusker yaimumunya Ingwe kama pipi
TIMU ya AFC Leopards Jumatano, Septemba 23 walipokezwa kichapo kizito cha 4-0 na mabingwa mara 11 Tusker FC kwenye mechi kali ya ligi iliyogaragazwa kwenye uga wa Kenyatta, Kaunti ya Machakos.
Vijana wa kocha Rodolfa Zapata walikuwa hoi mbele ya wapinzani wao vipindi vyote viwili vya mtanange huo huku udhaifu wao ukionekana wazi haswa katika safu ya ulinzi na mchumani.
Mabao ya Wanamvinyo hao wanaotiwa makali na mkufunzi wa zamani wa Leopards Robert Matano yalitikiswa wavuni na wanadimba Sydney Ochieng, Marlon Tangauzi, Boniface Muchiri na Jackson Macharia mtawalia.
Ulinzi wa Ingwe iliyovuja sana ilikuwa ikisitiriwa na wanasoka Mike Kibwage, Dancun Otieno (nahodha), Abdallah Salim na Baker Lukoya huku Ezekiel Owade akiaminiwa langoni kunyakia Ingwe ambao msimu huu wametoka mdomo kavu bila kubusu kombe lolote kinyume na mwaka jana(2017) walipotia kabatini ubingwa wa ngao ya Sportpesa.
Zapata ambaye alijitokeza kabla ya mechi na kusema kwamba habanduki Leopards jinsi uvumi ulivyoenea awali mtandaoni ulivyoashiria, alilenga kuwapa matumaini mashabiki wa timu hiyo haswa baada ya kubanduliwa katika mashindano ya Kombe la ngao Jumapili Septemba 23 na Mabingwa wa mwaka 2009, Sofapaka.
Wakiwa wamesalia na mechi mbili kabla ya kutamatika kwa msimu wa 2017/18, AFC Leopards watakuwa na kibarua kigumu kumaliza katika nafasi ya tatu, wakiwa wanakumbana na upinzani mkali kutoka kwa Sofapaka na Ulinzi Stars.