• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 7:55 PM
KAULI YA WALIBORA: Wanahabari waepuke uchale katika usomaji habari, wawaige mikota wa zamani

KAULI YA WALIBORA: Wanahabari waepuke uchale katika usomaji habari, wawaige mikota wa zamani

NA PROF KEN WALIBORA

KUNA taarifa za habari zilizokuwa zikisomwa na mkongwe wa usomaji habari, Khamis Themor wa VOK (baadaye KBC) zinazosambazwa kwa mtandao wa WhatsApp. Majuzi yale nilipita katika ofisi moja mjini Bungoma nikawakuta watu wamefungulia simu moja wanasikiliza taarifa za habari hizo.

Nikawauliza kama walikuwa wakisikiliza habari au historia. Wakajibu walikuwa wakisikiliza “historia.” Kwa kweli katika taarifa zilizokuwa zikisomwa ilikuwa dhahiri Rais Daniel arap Moi alikuwa bado rais wa Kenya. Nilishangazwa na uamuzi wa watu wazima hao kuketi na kusikiliza historia badala ya habari mubashara inayohusu maisha yao ya papahapa na sasa hivi.

Sikuisha kuwadadisi. Ndipo waliponiambia kwamba hizo taarifa za habari zilizosomwa na wakongwe kama Khamis Themor, Salim Juma, Anakilet Araba, James Njuguna, Willie Michael Mwangi, Jacob William Maunda, Anderson Kalu, Said Ali Matano, James Njuguna, Jack Oyoo Sylvester, ndizo habari hasa. Kwa nini nikauliza tena?

Wakajibu kwamba siku hizi habari ni mchezo au mzaha mtupu, hamna mazingatio wala umakinifu tena. Taarifa za habari za redioni na runingani zimegeuzwa sarakasi na uchale (comedy) wa kuchekesha watu, sio kuwapasha watu habari za hivi punde. Hilo sikulitarajia kutoka kwa mabwana wale.

Yaani watu wameamua kufuatia historia kuliko habari za hivi punde kwa sababu ya mabadiliko au mapinduzi yaliyotokea katika uwasilishaji wa taarifa za habari.

Nilipokuwa bado nimepigwa kibuhuti na hilo, niliwasikia wakitoa sababu ya pili ya kudorora kwa uwasilishaji wa taarifa za habari siku hizi. Walisema lugha ya redio na runinga ya kupeperushia habari ilikuwa safi na sanifu zamani zile. Ilivutia, ilikuwa na raghba.

Ulikuwa huwezi kuajiriwa kusoma taarifa ya habari kama umeathiriwa na lafudhi ya lugha yako asili, wala usingeandikishwa taarifa hizo ikiwa hukuwa umeimudu barabara lugha ya Kiswahili.

Waandishi wa habari waliziandika kwa ufasaha wa kuandika na kwa heba, wasomaji, kama Khamis Themor, wakazisoma habari hizo kwa ufasaha wa kusema na kusoma na kwa heba ya aina yake. Ilmuradi taarifa za habari zilitamanisha sio tu kwa lugha na uwasilishaji bali pia kwa kuchukuliwa kama kitu chenye mazingatio na unyeti.

Wasikilizaji wa historia walichupa mbele hadi kwa nyakati zetu hizi. Kwao wao hamna taarifa za habari tena zilizosalia. Uliopo ni upuuzi na mizaha na mparanganyo mtupu.

Wanasikitishwa na lugha duni inayotumiwa kuandika taarifa za habari. Aidha wanalalamikia usomaji holela wa habari, wasomaji hawazingatii kamwe kwamba ipo haja habari zieleweke na Kiswahili kieleweke. Wanasema kwa kasi ya umeme, jambo ambalo nimewahi kulidokezea katika safu hii hapo awali.

Taarifa ya habari imebaki tanbihi katika mpangilio mzima wa vipindi katika redio na runinga; kuna mambo muhimu zaidi kuliko kuwapasha watu habari za matukio na matokeo.

Kizazi cha sasa cha wanahabari hakina budi kujiuliza kwa nini watu wafuatie “historia” ilhali habari zipo. Pema hapo?

You can share this post!

Nilibandikwa jina ‘Sultan’ na maadui wangu,...

KAULI YA MATUNDURA: Kiswahili kinashuhudia mwamko mpya na...

adminleo