NYARIKI: Mtambo wa kusaga nafaka huitwa kinu wala si ‘kisiagi’
NA ENOCK NYARIKI
BAADHI ya watu hulitumia neno ‘kisiagi’ kwa maana ya mtambo wa kusaga nafaka. Kisiagi si neno rasmi la Kiswahili ila hutumiwa tu ili kufanikisha mawasiliano ya barabarani. Lipo neno kisaga ambalo yamkini limeundwa kutokana na sifa au tabia ya kitajwa ingawa halina uhusiano wowote na mtambo huo.
Kisaga ni mdudu wa rangi ya hudhurungi ambaye hutoboa mbegu kama vile maharagwe na kunde na kuzifanya kuwa na ungaunga. Fasiri ya Kiingereza ya kisaga ni ‘bean weevil’. Kitendo cha kutoa ungaunga kwenye mbegu ndicho yamkini kilichomfanya mdudu huyo kuitwa kisaga.
Zamani, kabla ya kubuniwa mtambo wa kisasa wa kusaga nafaka, nafaka zilitwangwa kwenye chombo mfano wa mtungi kilichoundwa kwa gogo.
Baadaye nafaka hizo zilizopondwapondwa zilipitishwa juu ya jiwe maalumu lenye umbo la tufe ili kuzisaga kuwa laini. Jiwe hilo lililotegwa ili kuinama kuelekea upande mmoja liliitwa kijaa.
Nafaka zilipoteleza juu ya jiwe lenyewe, zilikutana na jiwe jingine dogo ambalo lilipitishwa kwa nguvu juu ya jiwe kubwa kwa kutumia mikono yote miwili.
Kipo kile kilichokuja kujulikana baadaye kama ‘kinu cha maji’. Haya ni mawe mawili – moja juu ya jingine – yaliyotegwa kwenye mkondo wa mto wenye maji mengi ili kusaidia kusaga nafaka.
Mawe haya yalizungushwa kwa nguvu za maji kinyume na mawe ya kwanza ambapo jiwe dogo lilipitishwa juu ya lile kubwa kwa mikono. Sasa umebuniwa mtambo unaotumia diseli au nguvu za umeme.
Wanaolitumia neno ‘kisiagi’ kuurejelea mtambo huo wamelibuni kutokana na utenda kazi wa mtambo wenyewe. Hata hivyo, tulivyotangulia kusema, ijapokuwa neno hilo limetamalaki katika matumizi ya kila siku, si sanifu.
Neno sanifu na linalopaswa kutumiwa kuurejelea mtambo huo ni kinu. Msamiati huo una maana tatu ila maana mbili ndizo zinazohusiana na mjadala huu.
Maana ya kwanza ni chombo kama mtungi kilichoundwa kutokana na gogo ambacho hutumiwa kutwangia nafaka, mizizi au majani yatumiwayo kuwa dawa.
Chombo hiki ambacho hutumiwa pamoja na mti uitwao mchi ndicho tulichokitaja wakati tulipokuwa tukizungumza kuhusu kijaa au jiwe la kusaga nafaka. Maana ya pili ya neno kinu ni mtambo wa kutumia umeme au diseli utumiwao kusaga nafaka.
Kwa hivyo, neno sanifu linalopaswa kutumiwa kuurejelea mtambo wa kusaga mahindi ni kinu wala si ‘kisiagi’.