ONYANGO: EACC isijifiche kwa Biblia, iweke mikakati inayofaa
Na LEONARD ONYANGO
TUME ya Maadili na Kukabiliana na Ufisadi (EACC) kwa mara nyingine imejaribu kutumia neno la Mungu katika juhudi za kupambana na zimwi la ulaji hongo ambalo ni donda sugu humu nchini.
Tume ya EACC inayoongozwa na Askofu Mkuu mstaafu Eliud Wabukala, kwa ushirikiano na viongozi wa makanisa mbalimbali, wiki iliyopita ilizindua mwongozo wa masomo ya Biblia unaolenga kuwezesha Wakenya kuelewa anayosema Mungu kuhusiana na ufisadi.
Mwongozo huo pia unalenga kuhakikisha kuwa Wakenya wanasoma na kuelewa kwamba Mungu anachukia ufisadi hivyo kuwawezesha kuishi maisha ya uadilifu.
Wakati wa uzinduzi wa mwongozo huo, tume hiyo ilijitetea kwa kusema kuwa kila Mkenya ana jukumu la kuzuia au kukabiliana na ufisadi.
Hii si mara ya kwanza kwa EACC.Tume ya EACC mnamo Februari mwaka 2017 ilitangaza kushirikiana na viongozi wa kidini kutoka Baraza la Makanisa nchini (NCCK), Baraza la Dhehebu la Wahindu (HCK), Muungano wa Makanisa la Kiinjilisti (EAK) na Baraza Kuu la Waislamu (Supkem) kukabiliana na ufisadi nchini.
Tume ya EACC pamoja na viongozi hao wa kidini waliunda jopokazi la watu 12 ambalo lilitwikwa jukumu la kuhamasisha Wakenya kujiepusha na ufisadi.
Jopokazi hilo pia lilipewa jukumu la kuhimiza Wakenya kujiepusha na vurugu na kuchagua viongozi wenye maadili katika uchaguzi wa Agosti 8.
Jopokazi hilo la ‘watumishi wa Mungu’ lilifeli kwani juhudi zao ziliambulia patupu. Uchaguzi wa mwaka jana uligubikwa na fujo. Madai kwamba baadhi ya wabunge walichukua hongo ya Sh10,000 kila mmoja kutupilia mbali ripoti kuhusu kuingizwa kwa sukari ya magendo nchini inayodaiwa kuwa na sumu ni ithibati tosha kwamba hatukuchagua viongozi wenye maadili.
Wengi wa viongozi wafisadi waliapishwa kwa kutumia Biblia au Koran kabla ya kuanza kutekeleza majukumu yao katika afisi wanazoshikilia lakini hilo halijawazuia kuiba mali ya umma.
Idadi kubwa ya viongozi wanaokabiliwa na sakata za ufisadi wamekuwa wakihudhuria kila ibada katika misikiti na makanisani.
Tumeona wahubiri wa Injili wakinajisi watoto wadogo na hata kuhusishwa na sakata za wizi licha ya kuwa ‘wataalamu’ katika uchambuzi wa Neno la Mungu.
Ni kweli kwamba kila Mkenya ana jukumu la kupambana na ufisadi lakini EACC inafaa kufahamu kwamba wananchi wanalipa ushuru ili kuiwezesha kukabiliana na wezi wa fedha za umma.
Tume ya EACC haina budi kujiepusha na sarakasi na badala yake ikabiliane na ufisadi badala ya kuwabembeleza wafisadi kusoma Biblia ili wabadili mienendo yao.
Wafisadi hawana wakati wa kusoma Biblia kwani wanatumia muda wao mwingi kutafuta mianya na kuunda mipango ya kuiba fedha za Wakenya.
EACC inafaa kuwakamata na kuhakikisha kuwa wafisadi wanaadhibiwa badala ya kuwabembeleza kusoma Biblia.
Washukiwa wote wa ufisadi wanastahili kuchukuliwa hatua kulingana na sheria kwani fedha wanazopunja zingesaidia kupeleka nchi hii mbele zaidi kimaendeleo.