Haiwezekani kwa Pogba kutua PSG, Juventus au Barcelona. Hizi hapa sababu
Na CHRIS ADUNGO
UHUSIANO kati ya nyota Paul Pogba na mkufunzi wake kambini mwa Manchester United, Jose Mourinho ulielekea kusambaratika kabisa wiki iliyopita baada ya wawili hao kuzozana peupe wakiwa mazoezini. Tukio hilo limefasiriwa na wengi kuwa mwanzo wa mwisho wa kiungo huyo mzawa wa Ufaransa ugani Old Trafford baada ya kuvuliwa utepe wa unahodha.
JUVENTUS: Juventus, Paris Saint-Germain (PSG) na Barcelona ni baadhi ya vikosi vya soka ya bara Ulaya ambavyo huenda vikashawishika kwa sasa kumsajili Pogba. Hata hivyo, cha pekee ambacho kina uwezo wa kukwamiza uhamisho wa sogora huyo mwenye umri wa miaka 25 ni wingi wa fedha zitakazotakiwa na Man-United ili wamwachilie.
Tatizo zaidi ni uwezekano wa Pogba kutokubali kiasi chochote cha mshahara wa usiopungua Sh27 milioni ambazo kwa sasa anapokezwa na Man-United uwanjani Old Trafford kila wiki.
Kulingana na mwanahabari James Horncastle aliyewahi kumulika maisha ya Pogba kambini mwa Juventus, itawawia vigumu mno wapambe hao wa soka ya Italia kumrejesha Pogba kikosini mwao hasa baada ya kutumia zaidi ya Sh14 bilioni msimu huu ili kumshawishi Cristiano Ronaldo kubanduka Real Madrid, Uhispania.
Ingawa mkurugenzi wa Juventus, Beppe Marotta anavutiwa sana na utajiri wa kipaji cha Pogba, wadadisi wengi wa soka wanahisi kwamba halitakuwa jambo dogo kwa Juventus kumudu gharama ya kuwadumisha Ronaldo na Pogba jijini Turin.
PSG: Hali katika kikosi cha PSG si tofauti sana na ile ya Juventus. UEFA imeanzisha upya uchunguzi kuhusu matumizi ya fedha kambini mwa magwiji hao wa soka ya Ufaransa.
Msimu jana, PSG walimsajili Neymar kutoka Barcelona kwa hela zilizomfanya kuwa mchezaji ghali zaidi duniani. Walijinasia pia maarifa ya chipukizi Kylian Mbappe aliyerasimisha uhamisho wake kutoka Monaco kwa kima cha Sh23 bilioni.
Hata hivyo, mwanahabari wa Ufaransa Julien Laurens anahisi kuwa PSG huenda kwa sasa wasiwe katika uwezo wa kumudu mshahara wa Pogba ambaye atahitaji karibu Sh2.5 bilioni kwa mwaka.
Kulingana naye, uhamisho wa Pogba hadi PSG utawezekana tu iwapo atasalia ugani Old Trafford hadi Januari 2019 naye Neymar ashawishike kujiunga na Real Madrid muhula ujao.
BARCELONA: Mwanahabari mzawa wa Uhispania, Guillem Balague amesema kwamba Barcelona wapo radhi zaidi kumsajili Pogba ila wanahofia ukubwa wa bei iliyotolewa na wakala wake, Mino Raiola.
Barcelona wana uhusiano mbaya na Raiola ambaye aliwakashifu mno kwa kosa la kumwachilia Zlatan Ibrahimovic baada ya mwaka mmoja pekee wa kujivunia huduma zake.
Wakala huyo aliwahi kumgombeza mno kocha Pep Guardiola ka kutompanga Ibrahimovic kwenye kikosi cha kwanza cha Barcelona kilichotinga fainali ya UEFA mnamo 2011. Kwa kutotaka uhusiano wowote mwingine na Raiola, huenda Barcelona wakawa wepesi wa kumtwaa chipukizi wa Ajax, Frenkie de Jong.
Hata hivyo, safu ya kati ya Barcelona itakuwa thabiti hata zaidi iwapo watamsajili Pogba.