Pasta awapa waumini mvinyo badala ya divai
NA CORNELIUS MUTISYA
Misuuni, Machakos
Kioja kilishuhudiwa katika kanisa moja eneo hili pasta alipowanywesha waumini pombe akiwahadaa ilikuwa divai wakalewa chakari!
Kulingana na mdokezi wetu, waumini walikuwa wakikaribia meza ya Bwana, almaarufu ‘sakramenti’ kioja kilipotokea.
Siku ya kioja, waumini walifurika kanisani. Wanakwaya walianza ibada kwa kughani nyimbo zao rojorojo huku pasta akinyanyuka na kuanza kuwalisha chakula cha kiroho. Kila mmoja alihisi kubarikiwa mno.
Ilipotimu wasaa wa sakramenti, waumini walipiga magoti mbele ya madhabahu ili watimize wajibu huo muhimu wa imani.
“Mtumishi wa Mungu alizunguka akiwapa waumini kipande cha mkate na glasi iliyokuwa na divai,” alisema mdaku wetu.
Twarifiwa kwamba, pasta aliombea sakramenti na waumini wakateremsha mkate na divai. Baadhi ya waumini, na hasa wanawake walianza kutapika ovyo ovyo huku wengine wakiingiwa na hali ya kisunzi na wakaanza kusinzia.
Inadaiwa kwamba, waumini wote walianza kulewa na kuanza kubwabwaja maneno. Hata pasta hakusazwa, alianza pia kurukaruka mbele ya altari kama mja aliyepagawa na kupandwa na jazba.
Hakuna aliyekuwa akimsikiliza mwenzake. “Hali ilikuwa si hali mle kanisani. Kila mmoja alikuwa akifanya vituko kwa raha zake,” alisema mdaku wetu.
Inasemekana, wapita njia waliamua kujitoma mle kanisani kujua kilichojiri waliposikia kasheshe hiyo. Waliwapata waumini wakiwa hawajitambui na wakawakimbiza wale waliokuwa wamezidiwa katika dispensari ya karibu kupewa huduma ya kwanza.
Ripoti mtaani hapa zaarifu kwamba, muuguzi aliwashangaza wengi alipopima matapishi ya waathiriwa hao na kuwafichulia kuwa walikuwa wamekunywa pombe iliyokuwa na chembechembe ya methanol.
“Hawa watu wamekunywa pombe yenye methanol. Hata hivyo, hawako kwa hatari maana walibugia kiasi kidogo tu,” muuguzi aliwaambia waliofika na kuwashtusha mno.
Duru zaarifu kuwa, waumini hao walitibiwa na wakaruhusiwa kwenda nyumbani na siri ikafichuka kuwa pasta aliwapatia waumini pombe badala ya divai kisha akatoroka.