OBARA: Uboreshaji katiba wataka maarifa, si hisia
Na VALENTINE OBARA
MJADALA kuhusu mabadiliko ya katiba umezidi kushika kasi katika miezi ya hivi majuzi. Mdahalo huo ulikuwa umetulizwa tangu wakati Kiongozi wa Upinzani Raila Odinga aipoweka muafaka wa maelewano na Rais Uhuru Kenyatta mapema mwaka huu.
Tetesi za Bw Odinga zilihusu kuwezesha uchaguzi huru na wa haki baada ya uchaguzi uliopita, na sasa watetezi wamezinduka kufuatia kupitishwa kwa sheria ya fedha ambayo imeongeza ushuru wa bidhaa muhimu ikiwemo mafuta.
Mbali na Bw Odinga, wanaotaka marekebisho ya katiba ni viongozi wa kidini, chama cha Thirdway Alliance na baadhi ya wabunge.
Kile kinachofaa kueleweka ni kwamba marekebisho ya katiba ni suala zito ambalo linafaa kufanywa kwa makini.
Urekebishaji katiba ni shughuli inayotumia rasilimali nyingi za nchi na haifai kuchukuliwa kama jambo la mzaha la kutatua matatizo ya muda, bali iwe suluhisho la kudumu kwa changamoto za kitaifa.
Inavyoonekana kwa sasa, viongozi wanaopendekeza marekebisho haya wanatumia hisia za wananchi kuhusu hali ya maisha ili wapate kuungwa mkono na wengi.
Imekuwa jambo la kawaida sio Kenya pekee bali pia katika mataifa mengine mengi ulimwenguni kwamba katiba hurekebishwa tu wakati ambapo nchi inakumbwa na majanga ya aina mbalimbali.
Humu nchini, tulipata fursa ya kurekebisha katiba yetu punde tulipopata ukombozi kutoka kwa utawala wa mkoloni, kisha tukairekebisha tena katika mwaka wa 2010.
Marekebisho yaliyofanywa 2010 yalifanikishwa kufuatia ghasia za baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2007 ambapo watu zaidi ya 1,000 walifariki na maelfu wengine wakaachwa bila makao. Makovu ya ghasia hizo bado hutuandama hadi hii leo.
Kilichobainika katika kipindi hiki cha miaka minane ya katiba mpya iliyotuletea utawala wa ugatuzi ni kwamba tulifanya marekebisho kwa msingi wa hisia zilizotukumba wakati wa ghasia za 2007.
Tulikuwa na matarajio makubwa kwamba katiba hii ingetatua changamoto ambazo zilikuwa chanzo cha ghasia hizo za kikabila na zingine ambazo tulikuwa tumeshuhudia katika chaguzi zilizotangulia.
Ingawa ugatuzi umetatua baadhi ya changamoto zilizokuwa zikikabili wananchi mashinani, ni vigumu kuona mafanikio yoyote ambayo katiba hii imeleta kubadilisha mbinu za uongozi katika serikali kuu.
Bunge lililopaswa kuwa na mamlaka makubwa ya kutetea maslahi ya wananchi limeishia kutekwa na afisi ya rais.
Vile vile, lengo la kuleta uwakilishi sawa wa kijinsia serikalini limeishia kuletea mwananchi mzigo wa kugharamia mishahara mikubwa na marupurupu ya watumishi wa umma.
Zaidi ya hayo, mapendeleo ya kikabila katika kuajiri watumishi wa umma bado ni changamoto kubwa.
Licha ya haya, haitakuwa busara kuharakisha kubadilisha katiba wakati huu kwa kuchezea hisia za wananchi wanaotatizwa na hali ngumu ya maisha.
Tukifanya hivi tutarejea tena kwa wananchi hawa miaka michache baadaye tutakapogundua kwamba marekebisho yaliyofanywa hayakuzingatia hili na lile, bali yalikuwa tu ya kutimiza maslahi ya watu wachache wenye ushawishi mkubwa nchini.