• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 6:50 PM
Kipchoge amwomboleza kinara wa Nike aliyempa motisha

Kipchoge amwomboleza kinara wa Nike aliyempa motisha

Na GEOFFREY ANENE

NYOTA Mkenya Eliud Kipchoge amemwomboleza Naibu Rais wa kampuni ya vifaa vya michezo ya Nike, Alexander “Sandy” Bodecker, ambaye alimtaka atimke mbio za kilomita 42 chini ya saa mbili.

Bodecker, ambaye alifariki Oktoba 2 akiwa na umri wa miaka 66 baada ya kuugua ugonjwa wa saratani kwa muda mrefu, alikuwa na ndoto ya kuona binadamu akimaliza mbio za kilomita 42 kwa saa 1:59:59. Alijichora tatuu kwenye mkono wake wa kushoto muda huo.

Mwaka 2017, Bodecker aliwatafuta bingwa wa Olimpiki Kipchoge pamoja na Mwethiopia Lelisa Desisa na mshikilizi wa rekodi ya dunia ya mbio za kilomita 21, raia wa Eritrea Zersenay Tadese na kuwajumuisha katika mbio za kilomita 42 za Nike Breaking2 mjini Monza nchini Italia. Aliamini ushindani kati yao utawasukuma kutimka kilomita 42 kwa saa 1:59:59.

Ili kuwaandaa Kipchoge, Desisa na Tadese vilivyo kwa majukumu ya Breaking2, Bodecker aliwapangia ratiba ya mazoezi, masuala ya lishe na kuunda bidhaa za kuwasaidia kupata ufanisi huo.

Ingawa ndoto hiyo haikutimia wakati huo, Kipchoge alishinda mjini Monzao kwa saa 2:00:25, dakika 2:32 ndani ya iliyokuwa rekodi ya dunia wakati huo ya saa 2:02:57 ambayo Mkenya Dennis Kimetto aliweka jijini Berlin nchini Ujerumani mwaka 2014.

Muda huu haukutambuliwa kama rekodi ya dunia kwa sababu mbio zenyewe zilifanyika katika uwanja wa mbio za magari za langalanga, ambao haukuwa umefikia viwango vya Shirikisho la Riadha Duniani (IAAF).

Mwaka mmoja baadaye, Kipchoge ni mshikilizi wa rekodi ya dunia ya mbio za kilomita 42 za wanaume ya saa 2:01:39, ambayo aliweka akijishindia taji lake la tatu la Berlin Marathon mnamo Septemba 16, 2018.

Alitumia viatu spesheli vya kutimkia katika sehemu tambarare vya Nike Zoom Vaporfly, ambavyo vilitokana na ubunifu wa Bodecker. “Asubuhi hii (Oktoba 3, 2018) nimepokea habari za kuhuzunisha kwamba rafiki yangu Sandy Bodecker ameaga dunia.

Natumia familia yake, wapenzi wa michezo na kampuni ya Nike risala zangu za rambirambi. Bado siamini kifo chake. Nenda salama Sandy,” Kipchoge alichapisha katika mtandao wake wa Twitter.

Bodecker amekuwa katika kampuni ya Nike kwa miaka 36. Alijihusisha sana na soka na michezo kwa jumla na kuletea Nike sifa kubwa pamoja na mapato makubwa kutokana na kudhamini na kusambaza vifaa vya michezo.

You can share this post!

Alfred Keter na wenzake wamtaka Uhuru kuhakikisha wakulima...

Lango la JKIA kufungwa Melania Trump akitarajiwa kutua...

adminleo