MOKAYA: Mourinho ni kuku wa kuchinjwa
NA JOB MOKAYA
KUFUTWA kwa kocha wa Manchester United Jose Mourinho sasa ni suala la lini wala si iwapo. Kufutwa huko kunatokana na matokeo duni ambayo United inazidi kusajili.
Ingawa kumekuwa na habari kwamba Zinedine Zidane angetaka kuchukua nafasi ya Mourinho, hali hiyo imebadilika na sasa United inataka huduma za kocha wa Tottenham Mauricio Pochettino.
Manchester United ilishindwa na West Ham juma lililopita kwa kulazwa mabao matatu kwa moja na kisha kutoka sare ya bila kufungana na Valencia ya Uhispania kwenye mchuano wa Uefa Champions League kabla ya kujinyanyua na kuibwaga Newcastle United.
Matokeo haya duni yalifuatiwa na ushinde mwingine katika kombe la Carabao dhidi ya Derby County inayoongozwa na mchezaji wa zamani wa Mourinho Franc Lampard. Msumari kwenye kidonda ukiwa kwamba mechi yenyewe ilipigwa kwenye uga wa Old Trafford.
Mbali na matokeo duni uwanjani, Mourinho anajipata katika hali mbaya pale ambapo uhusiano wake na wachezaji wakuu timuni unapozidi kudorora.
Mathalani, uhusiano wake na Paul Pogba unazidi kuwa mbaya zaidi kiasi cha kupigana makonde. Mourinho na Pogba hawaangaliani uso kwa uso kutokana na tofauti zao.
Hali hii imemfanya Pogba kukiri mara kwa mara kwamba anataka kuondoka Old Trafford na kujiunga na klabu yake ya zamani ya Juventus au kujiunga na Barcelona inayomezea mate huduma zake.
Mwingine ni Alexis Sanchez aliyejiunga na Manchester United miezi michache iliyopiya kutoka Arsenal na ambaye hasemezani kabisa na Mourinho. Sanchez hajacheza mechi nyingi bila kuondolewa uwanjani na mchezaji mwingine kutwaa nafasi yake.
Hali hii imemfanya Sanchez kuona kwamba Mourinho hathamini mchango wake. Huenda Sanchez ana hoja yenye mashiko kwani katika mechi mbili tatu msimu huu, amekaa tu kwenye benchi.
Aidha, majarida mengine ya Uingereza kama vile The Sun na Mail Online Football, yamechapisha habari kwamba Mourinho hasemezani na nahodha wake ambaye ni Antonio Valencia.
Valencia amekuwa na mchango mkubwa kwenye timu akicheza upande wa kulia kama nambari mbili. Sehemu hiyo ndiyo imekuwa dhabiti zaidi timuni huku mabao machache tu yakitokea kwenye sehemu hiyo.
Uhasama wa Mourinho na Anthony Martial pia umekuwa kwenye darubini kwa muda sasa ambapo Martial amekuwa akitaka kuondoka Old Trafford ila hajafaulu kwani klabu itaenda hasara ikimuuza.
Hakuna timu inayotarajia kumnunua Martial kwa zaidi ya Pauni milioni 100 kwani hajakuwa akicheza katika mechi nyingi.
Mbali na Martial kuna wachezaji wengine wengi tu ambao watafurahi sana kuondoka kwa Mourinho. Na kwa Mourinho, atahitaji kuchukua likizo ya muda kutoka kwenye shughuli zote za soka hadi awe na mawazo sahihi ya kufunza. Kila la heri Mourinho uendako.