KAULI YA WALIBORA: Wahariri wana nafasi aali ya kuinua thamani na haiba ya Kiswahili
NA PROF KEN WALIBORA
TOVUTI ya kituo maarufu cha televisheni nchini mapema wiki hii ilikuwa na habari kuhusu “silaha za moto,” kauli ambayo sijawahi kuisikia katika lugha ya Kiswahili. Nilipigwa na butwaa sana kusoma habari hizo maana kwa kweli sijui ni nini kitu hiki kiitwacho “silaha za moto.”
Nikaanza utafiti mara moja na kuthibitisha tuhuma yangu kwamba mwanahabari na mhariri wake walikuwa wameboronga kama wanavyoboronga mara nyingi siku hizi.
Kauli yangu ni kwamba kuboronga Kiswahili ndiko uraibu wa Wakenya na hasa wanahabari. Unasikia makosa, unasoma makosa kila uchao kana kwamba hakuna chochote kingine cha manufaa kinachoweza kutekelezwa ila kufanya makosa.
Baada ya kuchangua kauli ya “silaha za moto” niligundua kwamba mwanahabari alikuwa anajaribu kutafsiri kauli ya Kiingereza “firearms,” yaani “bunduki.” Huu ndio mtindo wa kutafsiri kijinga na kizembe uliokita mizizi thabiti
Mkataa wangu ni kwamba huenda mwanahabari huyo alitaka kusema “bunduki” kama ni “firearm” ndilo lililokuwa neno la Kiingereza. Lakini kama nilivyotaja awali halikuwa kosa la mwanahabari aliyeandika habari ile tu; mhariri alipitwaje na taksiri hiyo?
Je, mhariri anapewa mshahara kufanya nini ila kusahihisha makosa ya uhakika, sarufi na mategu? Na anapopokea mshahara huku tunashuhudia lukuki ya makosa analala usingizi wake akiwa na dhamiri safi? Je, anakula na kunywa bila tashwishi?
Si mara ya kwanza mimi kulalamikia mtindo huu wa kutafsiri sisisi kivoloya. Mtindo huu ndio msingi mbaya wa kauli kama “usalama wa chakula” kuwa tafsiri ya “food security.”
Neno sahihi hapa ni utoshelevu wa chakula na kuwa na chakula cha kutosha. Lakini mifumo ya Kiingereza inapachikwa kwenye Kiswahili cha mparanganyo wa kutisha. Kila lugha ina kunga zake na muundo wake.
Kuna sababu kadha wa kadha za kuwepo kwa makosa mengi katika matini za Kiswahili katika vyombo vya habari. Kwanza hakuna thamani yoyote inayofungamanishwa na kusema na kuandika Kiswahili kizuri.
Angalia hali halisi uone kama watu wanajali kama unatongoa Kiswahili kizuri au kibaya. Nani anajali? Hukuona wakati mtoto wa mitaani aliposarifu Kiswahili kizuri Jaji Mkuu mstaafu Willy Mutunga alivyomchangamkia mpaka akala naye?
Kama mtoto huyu angesema Kiswahili kama mmoja mdogo zaidi kutoka Tanzania niliyomwona katika YouTube, matokeo yangekuwa yayo hayo? Sidhani. Ilmuradi hakuna thamani yoyote inayoambatanishwa na Kiswahili kizuri kwa hiyo mapuuza ndiyo yanayotawala matumizi ya Kiswahili.
Mfano mwengine ni taarifa za Safaricom zilizoratibiwa kiotomatiki. Utakuta unaletewa arifa “baki yako ya pesa ni ksh 5000.” Katika Kiswahili sahihi hatusemi “baki yako,” tunasema “baki lako.”
Lakini kampuni yenye mtaji na tija kubwa kama Safaricom haijali kuwatafuta wajuao Kiswahili vizuri waiandalie arifa zenye Kiswahili bora. Bora Kiswahili ni sawa kwao.
Ipo haja kupandisha thamani ya kusema na kuandika Kiswahili ipasavyo kama ilivyo kwa lugha nyingine za dunia. Njia moja ni kuajiri wahariri wazuri katika vyombo vya habari.