• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 2:10 PM
WANDERI: Je, Kibwana ndiye ‘Joshua’ wa kuikomboa Kenya?

WANDERI: Je, Kibwana ndiye ‘Joshua’ wa kuikomboa Kenya?

Na WANDERI KAMAU

SHINIKIZO za Wakenya kumtaka Gavana wa Makueni Kivutha Kibwana kuwania urais mnamo 2022 zinaonyesha mabadiliko makubwa ya kidhana ambayo huenda yakageuka kuwa msingi mkuu wa mwanzo wa mageuzi ya kisiasa nchini.

Kwa kipindi cha miaka mitano aliyohudumu kama gavana tangu 2013, Prof Kibwana ameonyesha maana tofauti ya uongozi, kinyume na ilivyo miongoni mwa dhana za Wakenya wengi.

Kwa Mkenya, maana halisi ya ‘uongozi’ ni uwepo wa magari makubwa, nyumba za kifahari, makumi ya walinzi na mambo mengine ‘makubwa makubwa.’

Kinaya cha haya ni kwamba dhana hii ni tofauti, hasa katika nchi na jamii zilizostawi kiviwanda. Katika nchi hizo, uongozi huchukuliwa kama utumishi kwa jamii. Viongozi huwa na mishahara midogo kwani kuwepo bungeni ama nafasi yoyote ya uongozi huonekana kama wito maalum kuihudumia jamii.

Katika Ugiriki ya zamani, wanafalsafa Socrates, Aristotle na Plato walitilia sana maanani maana ya uongozi, hali iliyowafanya kuanzisha chuo kikuu maalum cha kutoa mafunzo kuhusu uongozi.

Msingi wa mafunzo yao ulienea kote kote. Maeneo ambayo yalikumbatia mafunzo yao ni jamii zilizo katika maeneo ya Scandinavia, Ulaya Kaskazini na Asia Mashariki.

Baadhi ya nchi hizo ni Norway, ambayo licha ya kuwa na mfumo wa kifalme, uongozi huchukuliwa kama utumishi kwa manufaa ya jamii. Nchini Singapore, kiongozi wake wa kwanza, Lee Kuan Yew alisisitiza kwamba si lazima mtu ajitajirishe kwa kunyakua mali ya umma.

Kinaya kikuu barani Afrika kimekuwa kwamba uongozi hufasiriwa kama jukwaa la viongozi kupata ukwasi kujitajirisha na kuwa ‘miungu wadogo’ waabudiwao na wafuasi wao.

Hilo ndilo lilikuwa kosa la kwanza la msingi wa uongozi katika bara hii. ‘Ugonjwa’ huo umesambaa kiasi kwamba ni nchi chache sana barani ambazo zinatilia maanani uhalisia wa uongozi kama kigezo kikuu cha ustawi wake wa kisiasa, kijamii na kiuchumi.

Mkasa zaidi ni kwamba Kenya ni miongoni mwa waathiriwa wa ‘maradhi’ hayo. Msingi wetu wa uongozi ulitikisika tangu 1963, hali ambayo imetuzalia kila aina ya changamoto.

Huenda Prof Kibwana hatimaye ndiye ‘Joshua’ wa kutukomboa dhidi ya ukiritimba wa kisiasa kutoka familia chache? Je, 2022 ndio wakati huo? Wakenya ndio watakuwa waamuzi wakuu.

[email protected]

You can share this post!

Azua rabsha kipusa alipodinda kumnengulia kiuno

TAHARIRI: Umwagaji damu barabarani ukome

adminleo