• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
WAMALWA: Wakenya wajijengee viota vya maarifa kwa usomi wanaopata vitabuni na magazetini

WAMALWA: Wakenya wajijengee viota vya maarifa kwa usomi wanaopata vitabuni na magazetini

NA STEPHEN WAMALWA

KENYA ni nchi ya nne barani Afrika kuwa na idadi kubwa ya watu wanaojua kusoma na kuandika. Ripoti ya utafiti iliyochapishwa na shirika la The African Economist mwaka wa 2013, inaonesha kuwa nchi ya Zimbabwe inaongoza ikifuatiwa na Equatorial Guinea, Afrika Kusini kisha Kenya mtawalia.

Huenda hali ni bora zaidi kufikia sasa kutokana na juhudi za serikali kuendelea kutoa elimu bila malipo hasa kwa shule za msingi.

Hata hivyo, baada ya kupata ujuzi huu, je Wakenya wanautumia katika usomaji wa maandishi mbalimbali? Je, kuna faida ya taifa kuendelea kuwekeza katika juhudi za kuwasaidia watu wake kujua kusoma na kuandika?

Ukweli mchungu ni kuwa uzoefu wa kusoma miongoni mwa Wakenya hauridhishi. Ni nadra kuwapata Wakenya wakisoma magazeti, majarida, vitabu na maandishi ya aina nyinginezo.

Licha ya kuwa wengi wetu husafiri kwa muda mrefu barabarani, ni vigumu mno kumwona msafiri akisoma novela au kitabu kupitisha muda akiwa safarini. Utawakuta wengi wao kwenye mitandao ya kijamii wakisakura picha na video au wakibadilishana mawazo kwenye kumbi za mitandao. Wengine huazimia kulala usingizi wakisubiri kufika wanakokwenda.

Hatuna maeneo ambako watu wanaweza kupata vitabu kwa urahisi ikiwa watapenda kununua. Yapo maduka ya kuuza vitabu katika miji mikuu. Ila unapoanza kuingia maeneo ya vijijini, ni nadra kukutana na maduka au vibanda vya kuuza vitabu.

Sawa na shule za vijijini ambako utapata vitabu kwa nadra sana. Vilevile, wachuuzi wamezingatia sana bidhaa nyingine kama vile chakula kuliko kuchuuza maandishi.

Kwa wachache wanaouza vitabu, majarida au magazeti, biashara zao zina changamoto kubwa kwa kuwa hawachangamkiwi sana na wateja.

Wanafunzi katika taasisi za elimu wamekuwa watu wa kushangaza. Uchunzaji wa jinsi wanavyosoma unaonesha kuwa wengi wao husoma vitabu vinavyohusiana tu na masomo yao.

Wanadai kuwa hawana muda wa kusoma vitabu vingine nje ya taaluma yao. Waliokamilisha masomo yao katika ngazi mbalimbali za elimu wanadai kuwa waliufunga ukurasa huo wa kusomasoma na kuufungua mwingine wa kuyakabili maisha waliyo nayo sasa. Yaani, Wakenya wamebanwa na maisha eti. Hatuna maktaba za nyumbani. Ikiwa zipo basi utashangaa ukifahamu kuwa tunazitembelea kwa nadra sana.

Ni bora kufahamu kuwa usomaji unatuwezesha kujua maisha, mawazo na hata utamaduni wetu na wa watu wengine.

Kwa hivyo, huku kusomasoma kunaweza kutusaidia kutatua matatizo mengi yanayotukabili katika maisha ya kila siku. Si katika jamii tu bali pia katika afya, siasa na uchumi wetu.

Mwandishi ni mhadhiri wa Lugha ya Kiswahili na Fasihi ya Kiafrika, Chuo Kikuu cha Mafunzo ya Kigeni cha Tianjin, Uchina. [email protected]

You can share this post!

TAHARIRI: Umwagaji damu barabarani ukome

Babu Owino akaangwa kujilinganisha na Chamisa, Malema na...

adminleo