Makala

MKUU MPYA WA POLISI: Mchakato wa kujaza nafasi ya Boinnet waanza

October 14th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA

HUKU muda wa kuhudumu wa Mkuu wa Polisi Joseph Boinnet ukikaribia kukamilika, mchakato wa kujaza nafasi yake umeanza.

Boinnet ambaye aliingia afisini mnamo Machi 11, 2015 anapangiwa kustaafu ndani ya muda wa miezi mitatu ijayo, kulingana na Katiba.

“Inspekta Jenerali wa polisi atatueliwa na kuhudumu kwa muhula mmoja wa miaka minne na hawezi kuteuliwa tena kwa wadhifa huo,” inasema kipengee cha 245 (6) cha Katiba.

Maafisa wakuu serikalini wanaopangia kushawishi chagua la Rais Uhuru Kenyatta kwa wadhifa huo wameanza kushindania nafasi hiyo.

Wale wanaofahamu jinsi zoezi hilo huendeshwa wanasema kuwa uteuzi wa Inspekta Mkuu (IG) mpya hauhusu yule ambaye atasimamia huduma ya polisi pekee bali uteuzi huo pi utaongozwa na siasa.

Miongoni mwa wale ambao wanapigiwa upatu kumrithi Boinnet ni; Edward Mbugua, ambaye ni Naibu Inspekta Mkuu anayesimamia maafisa wa polisi na Noor Gabbow ambaye ni Naibu Inspekta anayesimamia Polisi wa Utawala.

Wadadisi  wanasema kuwa Rais Kenyatta pia huenda akateua mmoja wa maafisa wakuu wa usalama katika Ikulu, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kitaifa la Ujasusi (NIS) Philip Kameru au Mkurugenzi wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) George Kinoti.

Maafisa wakuu serikalini hata hivyo wanapigia debe aidha Mbugua au Gabbow wajaze pengo atakaloacha Bw Boinnet ambaye alipewa nafasi hiyo baada ya Bw David Kimaiyo kupigwa kalamu Desemba 31, 2014.

Mbungua na Gabbow walipewa nyadhifa zao mapema mwaka huu baada ya kupigwa kalamu kwa Joel Kitili (aliyekuwa Naibu IG aliyesimama polisi wa kawaida) na Samuel Arachi (Naibu Inspekta Jenerali aliyesimamia Polisi wa Utawala).

Inasemekana kuwa Bw Mbugua ana uhusiano wa kariu na Rais kwa sababu amewahi kuhudumu katika kikosi cha walinzi wa rais. Hata hivyo, maswali yameibuliwa kuhusu uteuzi wake ilhili umri wake umezidi miaka 55.

Akiwahutubia wakuu wa polisi katika Chuo cha Mafunzo ya Usimamizi Nchini (KSG) kule Kabete, Rais Kenyatta alikariri kujitolea kwake kufanikisha mabadiliko ambayo tayari yameanzishwa katika huduma ya polisi nchini (NPS).