• Nairobi
  • Last Updated March 19th, 2024 8:55 AM
Hazard nguzo tegemeo na mhimili tosha wa Chelsea

Hazard nguzo tegemeo na mhimili tosha wa Chelsea

Na CHRIS ADUNGO

EDEN Michael Hazard, 27, ni nyota mzawa wa Ubelgiji ambaye kwa sasa anavalia jezi za kikosi cha Chelsea nchini Uingereza. Ushawishi wa Hazard uwanjani huhisisika zaidi anapowajibishwa kama fowadi mvamizi au winga.

Ubunifu wake, kasi na uwezo wa kupiga chenga za maudhi na kudhibiti mpira ni miongoni mwa sifa zinazomweka katika orodha ya wachezaji wanaostahiwa pakubwa katika ulingo wa ulingo.

Akijulikana sana kwa uwezo wake wa kuchangia mabao na kukamilisha pasi za hakika kila anaposhuka dimbani, Hazard ameibukia kuwa kivutio miongoni mwa makocha wengi katika klabu maarufu za bara Ulaya.

Upekee wake katika usogora ni jambo ambalo linazidi kuwafanya baadhi ya wachezaji, makocha na wanahabari kuanza kuunasibisha uwezo wake na ule wa Lionel Messi na Cristiano Ronaldo ambao wametawala orodha ya washindi wa taji la Ballon d’Or ambalo hutolewa kila mwaka kwa Mchezaj Bora duniani.

Hazard amejipata aghalabu akiorodheshwa na wakufunzi, wachezaji wenza na watangazaji wa kabumbu kuwa miongoni mwa wanasoka bora zaidi katika ulimwengu wa kandanda.

Baada ya kipaji chake katika soka kutambuliwa katika umri mdogo, Hazard alisajiliwa na kikosi cha Lille nchini Ufaransa. Alihudumu katika kambi ya chipukizi wa kikosi hicho kwa miaka miwili kabla ya kuwajibishwa kwa mara ya kwanza mnamo Novemba 2007 akiwa na umri wa miaka 16.

Ukubwa wa kiwango cha utajiri wa kipaji chake ulimfanya kuwa sehemu muhimu katika kampeni za Lille chini ya ukufunzi wa kocha Rudi Garcia aliyemwajibishwa katika zaidi ya michuano 190 kati ya 2005 na 2012.

Katika msimu wake wa kwanza baada ya kujipa uhakika wa kuunga kikosi cha kwanza cha Lille, Hazard alitawazwa Chipukizi Bora na kuwa mchezaji wa kwanza asiye mzawa wa Ufaransa kulinyanyua taji hilo.

Mnamo 2009-10, Hazard alitawazwa mshindi wa tuzo hiyo kwa mara nyingine na kuingia katika mabuku ya historia kwa kuwa mchezaji wa kwanza kutia kapuni ubingwa wa taji hilo mara mbili. Katika msimu uo huo, Hazard aliteuliwa pia kuunga Kikosi Bora cha Mwaka katika kampeni za Ligue 1.

Mnamo 2010-11, Hazard alikuwa sehemu ya kikosi cha Lille kilichoshinda mataji mawili kwa mkupuo katika kampeni za soka ya Ufaransa. Ukubwa wa ushawishi na upekee wa mchango wake katika kampeni za msimu huo ulimchochea kutawazwa Mchezaji Bora wa Mwaka na hivyo kuwa mchezaji mchanga zadi kuwahi kutia kapuni taji hilo kwa mara ya pili mfululizo.

Ufanisi wake wa kijumla katika kampeni za msimu huo ulimfanya pia kupokezwa tuzo za haiba kubwa kutoka kwa majarida mbalimbali ya kimataifa, likiwemo la Guerin Sportivo nchini Italia.

Mnamo Juni 2012 baada ya kuhudumu kambini mwa Lille kwa zaidi ya miaka minane, Hazard alihamia kambini mwa Chelsea, Uingereza.

Katika msimu wake wa kwanza uwanjani Stamford Bridge, nyota huyo aliwachochea waajiri wake kutia kibindoni ubingwa wa Ligi ya Uropa kabla ya kutawazwa Chipukizi Bora katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) katika msimu wake wa pili.

Mnamo 2014-15, Hazard aliwachochea Chelsea kunyanyua ubingwa wa EPL na ufalme wa League Cup. Ufanisi huo ulimfanya kutawazwa Mchezaji Bora wa Mwaka na mchezaji aliyeimarika zaidi katika kampeni za msimu huo.

Miaka miwili baadaye, Hazard aliwasaidia Chelsea kunyakua ubingwa wa EPL kwa mara ya pili chini ya mkufunzi mzawa wa Italia, Antonio Conte mnamo 2016-17.

Hazard ambaye kwa sasa maarifa na huduma zake zinahemewa pakubwa na Real Madrid ni nahodha na tegemeo kubwa kambini mwa timu ya taifa ya Ubelgiji. Ubora wake umekuwa ukiimarika siku baada ya nyingine tangu awajibishwe kwa mara ya kwanza ndani ya jezi za Ubelgiji katika vikosi vya chipukizi wasiozidi umri wa miaka 17 na 19.

Hazard aliwajibishwa katika kikosi cha kwanza cha Chelsea kwa wachezaji wakomavu mnamo 2008 akiwa na umri wa miaka 17 pekee. Kibarua hicho ni mchuano wa kirafiki uliowakutanisha na Luxembourg. Yapata miaka mitatu baada ya kuwasakatia Ubelgiji mchuano wake wa kwanza, Hazard alifunga bao la kwanza ndani ya jezi ya kitaifa katika mchuano dhidi ya Kazakhstan mnamo Oktoba 2011.

Tangu wakati huo, amewajibishwa katika timu ya taifa zaidi ya mara 90 na alikuwa sehemu ya kikosi kilichotinga robo-fainali za Kombe la Dunia nchini Brazil mnamo 2014 kisha UEFA Euro mnamo 2016.

Katika fainali za Kombe la Dunia mnamo 2018 nchini Urusi, Hazard aliwaongoza wenzake akivalia utepe wa unahodha na kuchochea Ubelgiji kutua salama ndani ya mduara wa tatu-bora. Hiyo ilikuwa nafasi nzuri zaidi kwa Ubelgiji kuwahi kufikia katika historia yao ya kushiriki fainali za Kombe la Dunia.

Mchango wa Hazard katika fainali hizo za Kombe la Dunia ulimfanya kuibuka Mchezaji wa Pili Bora mwishoni mwa kipute hicho baada ya Luka Modric wa Croatia. Isitoshe, alijumuishwa katika orodha ya wachezaji 11-bora katika tuzo zilizotolewa na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) mnamo Oktoba 2018.

Hazard alizaliwa katika mji wa La Louviere na kulelewa viungani mwa jiji la Braine-le-Comte, Ubelgiji. Wazazi wake, Carine na Thierry, pia walikuwa wanasoka mahiri katika ujana wao.

Baada ya kuangika daluga zao katika ulingo wa kabumbu, wazazi wa Hazard walianza kuwa walimu wa soka. Thierry alistaafu rasmi mnamo 2009 ili awe na muda wa kutosha na wanawe.

Hazard ndiye mwanambee katika familia yao ya watoto wanne. Kaka zake pia ni wanasoka. Thorgan aliwahi kujiunga na Chelsea mnamo 2012 kabla ya kuyoyomea Ujerumani kuvalia jezi za Borussia Monchengladbach. Sogora huyo aliwahi pia kuchezea Lens ambao ni wakuu zaidi wa Lille nchini Ufaransa.

Kylian ambaye kwa sasa anachezea Chelsea, aliwahi kuvalia jezi za White Star Bruxelles na Ujpest. Ethan kwa sasa angali katika kademia ya kikosi cha Tubize, Ubelgiji.

You can share this post!

Angalia orodha ya Ballon d’Or ujue gani kali kati ya La...

Jombi aomba kanisa limsaidie kutimua mke

adminleo