SHERIA ZA MICHUKI: Maelfu ya magari kuondolewa barabarani
Na JOHN KAMAU
MAELFU ya magari ya uchukuzi wa umma yataondolewa barabarani kwenye operesheni kubwa itakayoanza Novemba 1, 2018.
Operesheni hiyo inalenga madereva, makondakta, polisi wa trafiki, wenye magari na kampuni za kujenga magari ili kurejesha kikamilifu “Sheria za Michuki”.
Wiki hii Serikali inatarajiwa kutangaza sera na kanuni mpya, na kuwapa wahudumu hadi Novemba 1, 2018 kuhakikisha wametekeleza kanuni hizo ikiwemo mikanda ya usalama, vidhibiti kasi na unifomu kwa madereva na makodkta.
Sasa pia itakuwa lazima kwa mashirika ya matatu na mabasi (Sacco) kuwapa ajira ya kudumu madereva, makodakta, mainspekta na mekanika wa magari yanayosimamia.
Operesheni hiyo pia inatarajiwa kuzima shughuli za magenge yanayosimamia sekta hiyo ya thamani ya mabilioni ya pesa.
Madereva wote wa matatu na makanga watakaguliwa upya kuhakikisha ni wale tu waliotimiza sheria za NTSA wanaoruhusiwa kuendesha magari ya kubeba abiria.
Shughuli hiyo ina lengo la kurejesha mfumo wa uchukuzi wa abiria wenye mpangilio sawa na ilivyokuwa wakati wa mabasi ya KBS miaka ya sabini na themanini. Mabasi hayo yalisukumwa nje na ushindani mkubwa kutoka kwa matatu.
Msako huo unaotarajiwa kushirikisha idara tofauti pia unalenga polisi wa trafiki na makundi yanayosimamia vituo vya matatu, ambao hudai hongo na ada haramu kutoka kwa wahudumu wa magari ya umma.
Hapo jana, maafisa wa ngazi za juu kutoka idara mbalimbali ikiwemo ile ya ujasusi (NIS), walifanya mkutano siku kutwa ili kukamilisha mipango ya operesheni hiyo ambayo duru zinasema itakuwa chungu kwa wenye matatu, wahudumu na hata abiria.
NIS imeshirikishwa katika operesheni hiyo ili iwe ikitoa habari kuhusu magenge ambayo yameteka sekta hii.
Duru zilisema mkutano wa jana ulihudhuriwa na Waziri wa Usalama Fred Matiang’i, Waziri wa Uchukuzi James Macharia, Katibu wa Usalama wa Ndani Karanja Kibicho, Katibu wa Wizara ya Uchukuzi Esther Koimet na Mkuu wa Polisi, Joseph Boinnet.
“Operesheni hii itakuwa kali, chungu na isiyosita hadi kuwe na utaratibu katika sekta hii,” Bw Kibicho aliambia Taifa Leo jana jioni.
Duru za kuaminika ziliambia Taifa Leo kuwa Rais Uhuru Kenyatta ameunga mkono operesheni hiyo kuendelea hadi mfumo wa uchukuzi wa umma ulainike.
Kwa sasa sekta ya matatu inasimamiwa na makundi yanayodai ada haramu kwa ufahamu wa polisi wa trafiki, ambao huhongwa na hawachukui hatua kwa wanaovunja sheria.
Kuna jumla ya magari 200,000 ya uchukuzi wa umma kote nchini, 20,000 kati ya hayo yakihudumu Nairobi.
Kampuni za kujenga matatu na mabasi pia zitalengwa kwenye operesheni hiyo ili kuhakikisha zinatilia maanani kanuni za NTSA.
Mabasi ya masafa marefu nayo yatahitajika kuwa na mashine za mfumo wa dijitali wa kuweka rekodi za kasi ya gari, na mahala iliyopo kila wakati.
Operesheni hii imekuja wiki moja baada ya basi kuua watu 56 katika eneo la Fort Ternan, Kaunti ya Kericho.