OBARA: Haisaidii kusubiri ajali ndipo sheria zitekelezwe
Na VALENTINE OBARA
RIPOTI kuwa serikali inapanga kuanzisha msako mkali dhidi ya wakiukaji wa sheria za barabarani ilipokelewa vyema na wananchi wengi.
Hii ni hatua ambayo imekuwa ikisubiriwa kwa muda mrefu na kila mmoja ambaye amechoshwa na jinsi maisha ya wananchi yamekuwa yakipotea kiholela katika ajali za mara kwa mara za barabarani.
Licha ya haya, hatuwezi kusahau kwamba haitakuwa mara ya kwanza kwetu kushuhudia haya.
Imekuwa kama desturi kuona asasi za serikali zinazohusika na utunzaji wa usalama barabarani zikikaza kamba kutekeleza sheria za uchukuzi baada ya ajali mbaya kutokea. Haya yamewahi kushuhudiwa katika miaka iliyotangulia.
Wakati huu, mipango ya kuimarisha usalama barabarani imetangazwa baada ya ajali iliyotokea katika Kaunti ya Kericho ikihusisha basi lililokuwa likielekea Kakamega ambapo watu zaidi ya 50 walifariki.
Asasi za serikali, hasa idara ya polisi wa trafiki na Mamlaka ya Kitaifa ya Usalama na Uchukuzi (NTSA) ni sharti ziwajibike kutekeleza sheria za barabani kikamilifu kila mara badala ya kusubiri ajali mbaya zitokee.
Huenda ikawa ukaguzi wa magari hufanywa ipasavyo lakini punde ukaguzi huo unapokamilika na gari kuruhusiwa kuhudumu, wamiliki au wahudumu huvuruga vifaa muhimu vya kuhakikisha usalama kwa abiria kama vile vidhibiti mwendo.
Vile vile, vyama vya ushirika vya matatu almaarufu kama SACCO vinaweza kuthibitishiwa magari yao yanastahili kuwa barabarani lakini baadaye yanaenda kuongeza magari yasiyostahili kuhudumu.
Hii ina maana kuwa jukumu kubwa la kuhakikisha sheria za barabarani zinatekelezwa liko mikononi mwa polisi wa trafiki.
Ufisadi
Tatizo lililopo ni kuwa ulaji rushwa kwa polisi wa trafiki ni jambo lililo wazi lakini halionekani kuwa litakomeshwa hivi karibuni.
Hili ni tatizo linalopaswa kukomeshwa kupitia kwa njia yoyote ipasayo kama kweli serikali imejitolea kusitisha maafa yanayotokea barabarani.
Upekuzi ambao umewahi kufanywa na wanahabari umeonyesha kuwa mlungula unaopokewa barabarani na polisi huwafikia wakubwa wao. Hapa ndipo kuna changamoto, kwani wale wakubwa wanaotarajiwa kuadhibu walio chini yao ni washirika katika rushwa.
Kinachosikitisha ni kuwa haya yanaendelea hata baada ya pesa nyingi za mlipa ushuru kutumiwa kupiga msasa maafisa wa polisi ambapo tuliambiwa wale waliokuwa wamekosa uadilifu walichujwa kutoka kikosini.
Sheria tulizo nazo kwa sasa za barabarani zina nguvu mno kulinda maisha ya wasafiri, lakini tunachohitaji ni viongozi wakakamavu ambao watakerwa na kila ajali inayotokea ndipo wajikakamue kuhakikisha ajali hizo zimepunguzwa kabisa.
Hakuna haja kwa maafisa husika kujifanya wanatekeleza sheria kikamilifu tu baada ya ajali mbaya kutokea kisha wanarudi usingizini baada ya muda mfupi.
Mbali na haya, abiria pia wana jukumu la kulinda maisha yao wenyewe. Hatua kama vile kutokubali kupanda gari lililojaa au kupiga ripoti kuhusu dereva anayeendesha gari kwa kasi kupita inavyohitajika zinaweza kusaidia kuokoa maisha ya wenzetu.