Inavunja moyo kuona viongozi vijana wafisadi – Uhuru
RUTH MBULA Na BENSON MATHEKA
RAIS Uhuru Kenyatta Jumatatu aliwaingilia vijana walio katika nafasi za uongozi akisema wale waliokabidhiwa nyadhifa mbalimbali wamemvunja moyo yeye mwenyewe na taifa lote kwa jumla.
Akihutubu katika eneo la Sotik, Kaunti ya Bomet alipofungua kiwanda cha maziwa, Rais Kenyatta alisema vijana waliopewa nafasi za uongozi wameshindwa katika majukumu yao na kuwa ndio wanaoongoza katika ufisadi.
Aliongeza kuwa vijana hao hawana cha kuonyesha katika vyeo walivyopewa na akawatetea wazee akisema wamekuwa wakifanya kazi bora na ya kuridhisha wakilinganishwa na vijana, na pia wanazingatia maadili.
Rais alisema vijana wengi hulalamika kila mara kuhusu uhaba wa nafasi za kazi lakini wanashindwa kutumia fursa wanazopewa.
“Kila mara wanahimiza viongozi wazee kuondoka kwenye vyeo, lakini tukitazama mahala walipo vijana, tunaona shida tupu,” akasema
Aliwapatia changamoto vijana kuchukua fursa ya vyeo wanavyopewa kuonyesha wanaweza kufanya kazi inavyohitajika na pia wanaweza kutegemewa.
Kumekuwa na malalamiko katika teuzi ambazo Rais amekuwa akifanya vijana wakilalamika kuwa anapendelea wazee.
Rais alionekana kuwalenga magavana vijana ambao kaunti nyingi wanazosimamia zinakumbwa na matatizo na siasa duni.
Lakini ikiwa Rais Kenyatta alimaanisha maafisa wa serikali walioshtakiwa kwa ufisadi, wazee waliofikishwa kortini ndio wengi.
Tangu atangaze vita dhidi ya rushwa, maafisa wa wizara, idara na mashirika ya serikali walioshtakiwa kwa ufisadi ni walio na umri wa zaidi ya miaka 35 ambao kulingana na Katiba hawawezi kuitwa vijana.
Maafisa wa Shirika la Vijana wa Huduma kwa Taifa (NYS), Hazima ya Vijana, kampuni ya stima nchini (Kenya Power) na Shirika la ukadiriaji ubora wa bidhaa nchini (KEBS) walioshtakiwa kwa ufisadi wako na umri wa zaidi ya miaka 40.
Katika Baraza la Mawaziri hakuna waziri aliye na umri wa chini ya miaka 40. Mawaziri wanaohudumu kwa sasa wako na umri wa kati ya miaka 46 na 60.
Miongoni mwa waziri wenye umri wa chini ni waziri wa Kilimo Mwangi Kiunjuri aliye na umri wa miaka 49, Eugene Wamalwa aliye na umri wa miaka 49, Charles Keter (Kawi) aliye na umri wa miaka 48 na Joe Mucheru, waziri wa Tekinolojia ya Habari na Mawasiliano ambaye ana umri wa miaka 46.
Huenda ikawa Rais alikuwa akizungumza kuhusu vijana kwa kutozingatia umri unaowafafanua kikatiba, na badala yake wale wanaoonekana vijana machoni pa umma.