Kipchoge, Cheruiyot, Korir na Chepkoech Tuzo ya Mwanariadha Bora Duniani
Na GEOFFREY ANENE
WAKENYA Eliud Kipchoge, Timothy Cheruiyot, Emmanuel Korir na Beatrice Chepkoech watawania Tuzo ya Mwanariadha Bora Duniani mwaka 2018.
Shirikisho la Riadha Duniani (IAAF) limeweka mshikilizi wa rekodi ya dunia ya mbio za kilomita 42 duniani Kipchoge (saa 2:01:39) na washindi wa Riadha za Diamond League Timothy Cheruiyot (mbio za mita 1,500) na Korir (mbio za mita 800) katika orodha ya wawaniaji 10 wa Tuzo ya Mwanariadha Bora mwanamume.
Mmoja kutoka orodha ya Kipchoge, Cheruiyot na Korir na Waamerika Christian Coleman (mbio za mita 60 & mita 100) na Noah Lyles (mita 150, mita 200 & mita 4×100), Mswidi Armand Duplantis (kuruka kwa fito), raia wa Afrika Kusini Luvo Manyonga (kuruka umbali), Mfaransa Kevin Mayer (heptathlon & decathlon), raia wa Qatar Abderrahman Samba (mita 400 kuruka viunzi & mita 4×400) na Tomas Walsh kutoka New Zealand (kurusha tufe), atatawazwa mwanariadha bora wa mwaka mwanamume.
Chepkoech, ambaye ni mshikilizi wa rekodi ya dunia ya mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji (dakika 8:44.32), atashindania taji la wanawake dhidi ya Dina Asher-Smith (Uingereza), Sifan Hassan (Uholanzi), Caterine Ibarguen (Colombia), Mariya Lasitskene (Authorised Neutral Athlete), Shaunae Miller-Uibo (Bahamas), Sandra Perkovic (Croatia), Caster Semenya (Afrika Kusini), Nafissatou Thiam (Ubelgiji) na Anita Wlodarczyk (Poland).
Shughuli ya kupigia wawaniaji wanawake kura ilianza Oktoba 22 nayo ya wanaume imeanza Oktoba 23. Zoezi hili la upigaji kura litakamilika Novemba 12 (wanawake) na Novemba 13 (wanaume).
Baada ya zoezi hili, wawaniaji watapunguzwa hadi tano katika vitengo vyote viwili kabla ya washindi kutangazwa mjini Monaco mnamo Desemba 4, 2018.