KAULI YA WALIBORA: Tukome kubeba dhana za Kiingereza kivoloyavoloya na kuzipachika katika Kiswahili
NA PROF KEN WALIBORA
Nini maana ya “kuokoa uso” katika Kiswahili? Hakuna au kama maana hiyo ipo ni maana duni kabisa. Lakini nilipitia makala moja ya Kiswahili nikakutana na kauli hiyo iliyonipiga kibuhuti.
Hata hivyo, uzoefu wangu mdogo wa sentensi za ajabu ajabu katika Kiswahili umenionesha kwamba aghalabu tatizo hili hutokana na tafsiri mbaya kutoka kwa Kiingereza.
Nimesema hapa mara nyingi na bado nitaendelea kusema kwamba, tafsiri sisisi kutoka kwa Kiingereza hadi kwa Kiswahili huzua mtafaruku mkubwa kilugha.
Nataka nieleweke vizuri. Tafsiri sisisi na utohozi ni sehemu ya ukuzi wa lugha zote duniani. Michakato hiyo ya kiisimu ina pahala pake na miktadha yake. Hata hivyo ipo mipaka katika matumizi yake.
Sisi katika Kiswahili, mathalani tunaposema “kupiga kura,” “kupiga pasi,” na “kupiga kamsa,” wasemaji wa Kiingereza wataeleza dhana hizo zote bila kutumia “piga” katika lugha yao.
Kwao kauli hizo zitakuwa “to vote,” “to iron”, na “to raise alarm.” Neno “kupiga” au “piga” la Kiswahili limepotea katika dharura ya mfumo wa kisintaksia na kisemantiki wa Kiingereza. Limepotea ili maana isipotee wakati dhana imehawilishwa kutoka kwa Kiswahili hadi kwa Kiingereza.
Kwa nini basi sisi watumiaji wa Kiswahili wameingia katika mtego wa kujitakia kunaswa kwa kufikiria ni lazima wabebe dhana za Kiingereza neno kwa neno na kuzipachika katika Kiswahili?
Je, hatujui kwamba tunapobeba dhana neno kwa neno kutoka katika lugha nyingine, tunabaki na maneno bila dhana? Tunakuwa tumevunja kabisa uhusiano ya kimaana kati ya lugha chanzi na lugha lengwa.
Yaani tunachotimiza katika ukasuku wetu usiokuwa na makini wala macho ni kwamba tunabeba maneno ya lugha nyinginezo na kuacha maana kuko huko.
Maana ambayo ndiyo tunapaswa kuihamisha inabaki kuko huko katika lugha chanzi, au inakwenda arijojo mfano wa tiara kwenye uwanda wa kizakiza kati ya lugha hiyo ya awali na lugha lengwa.
Prof Hermas Mwansoko wa Tanzania amefafanua kwa kina faida na hasara ya tafsiri katika kazi zake nyingi kuhusu tafsiri. Labda la kuzingatiwa zaidi hapa ni kauli yake na wenzake katika kitabu chao Tafsiri na Ukalimani kwamba “Tafsiri ni zoezi la uhawilishaji (transferring) wa mawazo katika maandishi kutoka lugha moja hadi lugha nyingine.” Ni kuhamisha “mawazo” sio maneno na hapo ndipo wengi wetu tunapokanyaga chechele au kupotea njia.
Nasisitiza kwamba tafsiri sisisi au neno kwa neno ina mahala pake. Mathalan sentensi “He climbed a tree” inaweza kutafsiriwa kwa Kiswahili kuwa “Alikwea mti” ingawa hata hapa kiwakilishi cha jinsia “he” hakiwezi kuwasilishwa kwa Kiswahili kikamilifu. Lakini angalao hapa tafsiri ya moja kwa moja inawezesha maana kuhamishwa kutoka kwa Kiingereza hadi kwa Kiswahili.
Lakini “kuokoa uso” tunauokoaje katika Kiswahili? Je uso umekabiliwa na tishio la kuchomwa maji moto au kuzabwa konde la Mike Tyson? Nimeachwa nimeachama.